uraha Samweli Ligate (26) mkazi wa kijiji cha Unyangala wilaya ya Makete
mkoani Njombe amehukumiwa kifungo cha miaka 30 jela kwa kosa la kumbaka
mara mbili mtoto mwenye umri wa miaka 15 aliyekuwa amehitimu darasa la 7
mwaka 2021 akisubiri kujiunga na kidato cha kwanza mwaka huu wa 2022
Hukumu
hiyo imetolewa na mahakama ya wilaya ya Makete mbele ya hakimu mkazi wa
Mahakama hiyo Mh.Ivan Msacky na mwendesha mashitaka Inspekta Msaidizi
wa Polisi (Asistant Inspector) Benstad Samson Mwoshe
Imeelezwa
kuwa bila halali mshtakiwa huyo alitenda kosa hilo la ubakaji Desemba
24, 2021 majira ya saa 12 jioni na kurudia tena Desemba 25, 2021 kinyume
na kifungu cha 130 (1)(2)(e) kikisomeka pamoja na Kifungu cha 131(1)
vya Sheria ya Kanuni ya Adhabu Sura ya 16 kama ilivyofanyiwa marejeo
mwaka 2019
Mshtakiwa huyo anadaiwa kumwita chumbani kwake mtoto
huyo ambaye anamwita mshtakiwa mjomba na kumbaka kisha kumtishia
kumdhuru endapo angesema kwa mtu yeyote kama amefanyiwa kitendo hicho na
mtoto huyo alishindwa kuvumilia na kutoa taarifa ambapo mshtakiwa
alikamatwa na hatua zikachukuliwa hadi kesi hiyo ilipofikishwa
mahakamani na pia mtoto huyo alipofikishwa hospitali kwa uchunguzi
iliguundulika kuwa ameingiliwa kimwili na ni mjamzito
Mwendesha
mashitaka wa serikali Inspekta Msaidizi wa Polisi Benstard Mwoshe
ameiomba mahakama hiyo kutoa adhabu kali kwa mshtakiwa ili iwe fundisho
kwake na kwa watu wengine kwani kitendo kilichofanywa na mshtakiwa ni
cha kikatili na kimemuathiri mtoto pamoja na kukatisha ndoto zake za
kimasomo
Akizungumza mahakamani hapo kabla ya hukumu kutolewa
mshtakiwa huyo ameiomba mahakama hiyo imuonee huruma na kumpunguzia
adhabu kwa kuwa ana familia inayomtegemea ikiwemo mama yake mzazi ambaye
ni mzee pamoja na watoto watatu ambao wanamtegemea na amewaacha bila
utegemezi wake
Hakimu Mkazi Msacky amesema mahakama hiyo
imezingatia maombi ya mshtakiwa ya kupunguziwa adhabu hivyo mahakama
hiyo imemtia hatiani kwa kosa la ubakaji na kumhukumu kifungo cha miaka
30 gerezani.