Mwandishi wa habari na mpiga picha wa kituo cha Fox News, Pierre Zakrzewski aliyekuwa na umri wa miaka 55, ambaye alikuwa na makazi yake jijini London, ameuawa katika shambulio la majeshi ya Urusi katika Mji wa Horenka, nje kidogo ya Mji Mkuu wa Kyiv nchini Ukraine.
Akimzungumzia mwandishi huyo ambaye ameacha mke na watoto watatu wa kike, Mkurugenzi wa Fox News, Suzanne Scott amemuelezea marehemu kama mwandishi shujaa ambaye alifuata miiko ya kazi zake na kueleza kwamba mkewe na wanaye, walikuwa wakisubiri mwili wa mpendwa wao jijini London.
Mkurugenzi huyo amesema Zakrzewski alikuwa tegemeo kwani aliripoti kwa ufasaha kutoka maeneo yenye vita ikiwemo Iraq, Afghanistan, Libya, Somalia, Palestina na Syria na kuongeza kwamba siku zote alisimamia weledi wa kazi yake.