Mshtakiwa amuogopa Sabaya asema ni mtu hatari

Shahidi wa saba upande wa utetezi katika kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya, Watson Mwahomange (27) ameiomba Mahakama impatie ulinzi gerezani kwa madai kuwa “Sabaya ni mtu hatari.”

Hata hivyo, Hakimu anayesikiliza kesi hiyo, alimtaka awasilishe ombi hilo kwa uongozi wa Gereza la Kisongo na ukiona kuna haja ya kufanya hivyo watafanya.

Mwahomange ambaye pia ni mshtakiwa wa tatu katika kesi hiyo ambaye jana alianza kujitetea mwenyewe baada ya aliyekuwa wakili wake kujitoa, aliyasema hayo jana mahakamani mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi Patricia Kisinda.

Alipoanza utetezi wake, aliiambia mahakama kuwa anafahamiana na Sabaya tangu 2019 baada ya kumpatia kazi ya kumpiga picha akiwa katika ibada iliyofanyika Kanisa la KKKT, Azimio iliyohudhuriwa na Askofu wa Kanisa hilo Dayosisi ya Kaskazini Kati, Dk Solomon Masangwa na mfanyabiashara maarufu jijini Arusha, Mchungaji Philemon Mollel.

Alisema alishindwa kuachana naye (Sabaya) kwa sababu alikuwa kama mateka wake na alihofia usalama wa maisha yake.

Alidai kutokana na hofu aliyokuwa nayo, alishindwa kwenda kuripoti mahali popote kuhusu tukio lililotokea kwa Mrosso.

Alipoulizwa na Hakimu Kisinda iwapo anafahamu mashtaka yanayomkabili, mshtakiwa (shahidi) alijibu ndiyo anayafahamu ni mawili huku akiyataja kuwa ni pamoja na la kuunda genge la uhalifu na utakatishaji fedha Sh90 milioni kutoka kwa mfanyabiashara Mrosso.

Aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya amekana kuwafahamu watuhumiwa wenzake watano kati ya sita katika kesi ya uhujumu uchumi huku akidai kuwa alitumiwa watu wa kumuua.


Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii