WAKATI wakihatarisha maisha yao katika mapambano dhidi ya Ebola nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), wanawake wanaoshiriki katika mazishi salama na ya heshima ya waathirika wa ugonjwa huo wanakabiliwa na unyanyapaa, vitisho na dhana potofu kutoka kwa jamii zinazowazunguka.
Miongoni mwa wanawake hao ni Chimene Mwanaki, ambaye ni mwanachama wa kikundi kinachoratibu mazishi ya wagonjwa waliofariki kwa Ebola kwa kuzingatia taratibu za usalama na heshima.
Mwanaki anasema baadhi ya wanajamii huwanyanyapaa wanawake wanaofanya kazi hiyo, wakidai kuwa wanaweza kuwaambukiza waume zao au kushindwa kupata wenza wa ndoa kutokana na dhana kwamba wao ndio wanaosambaza ugonjwa huo.
“Baadhi ya watu wanatuambia kuwa tunaweza hata kuua waume zetu kupitia maambukizi au kwamba hatutapata mtu yeyote wa kutuoa, kwa sababu wanafikiri sisi ndio tunaosambaza Ebola, ingawa sivyo ilivyo,” anasema Mwanaki.
Hali hiyo inaendelea licha ya juhudi za kukabiliana na ugonjwa huo, ambao miezi sita tangu kutangazwa kwa mlipuko wake nchini humo bado unaendelea kusababisha maambukizi na vifo.
Kwa mujibu wa takwimu za serikali zilizotajwa katika taarifa hiyo, zaidi ya maambukizi 11,000 yalikuwa yameripotiwa, huku karibu nusu ya walioambukizwa wakifariki dunia.
Mlipuko huo umetajwa kuwa mbaya zaidi kati ya milipuko 17 ya Ebola iliyowahi kutokea nchini DRC, huku ukiwa katika hatari ya kuzidi idadi ya vifo vilivyosababishwa na mlipuko wa Afrika Magharibi kati ya mwaka 2014 na 2016, ulioua takribani watu 11,000.
Katika juhudi za kudhibiti maambukizi, mpango wa Mazishi ya Heshima na Salama (DSB) umeunda timu za kushughulikia miili ya waliofariki katika maeneo ambayo hayana timu rasmi za mpango huo.
Timu hizo za kijamii zinajulikana kama ECUMAIR, zikiwa na jukumu la kuhakikisha mazishi yanafanyika kwa kuzingatia taratibu za usalama na heshima.
Wakati mlipuko huo ulipotangazwa katikati ya Mei, tayari watu 43 walikuwa wameripotiwa kufariki kutokana na Ebola, hali iliyoashiria kuwa virusi hivyo vilikuwa vimeenea kwa muda bila kugundulika.
Tangu wakati huo, ugonjwa huo umeenea katika mikoa minane kati ya 26 ya DRC, huku maeneo mapya yakiendelea kuripoti maambukizi na kuongeza mzigo kwa mfumo wa huduma za afya.
Msimamizi wa mpango wa DSB katika eneo la afya la Oicha, Jean Manina, anasema hufuatilia utekelezaji wa majukumu ya timu hizo ili kuhakikisha taratibu za mazishi zinafuatwa, ikiwemo namna wanavyovua vifaa vya kujikinga baada ya kumaliza kazi.
Anasema kila siku huanza kwa kupitia taarifa za ufuatiliaji wa maambukizi na kutembelea maeneo yenye timu za ECUMAIR ili kukagua utendaji wake.
“Tunapopata taarifa kutoka eneo la afya ambako tuna timu ya ECUMAIR, lazima niende huko kuona jinsi wanavyotekeleza majukumu yao,” anasema Manina.
Anaongeza kuwa katika maeneo ambayo hayana timu hizo, timu ya dharura inayohamishika ndiyo hutumwa kushughulikia mazishi.
Hata hivyo, kazi hiyo inawaweka wanachama wa timu hizo katika mazingira magumu, si kwa sababu ya hatari ya kuambukizwa Ebola pekee, bali pia kukosa muda wa kutosha kuwa na familia zao na kukabiliwa na mashambulizi ya maneno kutoka kwa wanajamii.
Baadhi ya watu huwatuhumu kuwa wanaharibu miili ya marehemu kutokana na utaratibu wa kuchukua sampuli za miili hiyo ili kubaini kama Ebola ndiyo iliyosababisha kifo.
Manina anasema unyanyapaa huo hauishii katika maeneo wanayofanyia kazi, bali pia unaendelea katika mitaa wanayoishi, ambako baadhi ya majirani huwadharau na kuwatuhumu kuwa wanafaidika kifedha na vifo vya wananchi.
“Tunapokuwa nyumbani, majirani zetu hutuambia kuwa sisi ni sehemu ya juhudi za kukabiliana na ugonjwa huu, hivyo tunapata pesa na kuwawezesha wazungu kuua raia wenzetu. Hata hivyo, hilo si kweli. Tunapambana ili kutokomeza maambukizi ya Ebola,” anasema Manina