Doue sasa kupasuliwa goti

KLABU ya Paris Saint-Germain imethibitisha kuwa mshambuliaji wake, Désiré Doué, atafanyiwa upasuaji baadaye mwezi huu baada ya kuumia goti la kulia mwishoni mwa wiki.

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 21 alipata jeraha hilo katika mchezo wa Ligi Kuu Ufaransa, Ligue 1, dhidi ya Nice uliochezwa Jumamosi usiku, ambapo PSG ilishinda kwa mabao 3-2.

Doué aliumia mwishoni mwa kipindi cha kwanza baada ya goti lake la kulia kupinda vibaya wakati akikimbia bila kuguswa na mchezaji mwingine. Alionekana akiwa katika maumivu makali na baadaye alibebwa kwa machela huku akilia.

Tukio hilo lilifanya mchezo usimame kwa takribani dakika tano huku madaktari wakitoa huduma kwa mshambuliaji huyo kabla ya kuondolewa uwanjani kwa makofi kutoka kwa mashabiki waliokuwa kwenye Uwanja wa Allianz Riviera.

Jeraha hilo ni pigo kubwa kwa PSG, hasa kwa sababu Doué alikuwa miongoni mwa wachezaji waliokuwa wakifanya vizuri zaidi msimu huu.

Mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Ufaransa alikuwa na mchango mkubwa katika kikosi cha PSG kabla ya jeraha hilo, lakini sasa atalazimika kukaa nje kwa muda mrefu kutokana na tatizo hilo la goti.

Doué pia amekuwa na historia ya matatizo ya majeraha. Msimu wa 2025/26 alikosa michezo 13 kutokana na majeraha ya misuli ya paja.

PSG imekuwa ikikumbwa na tatizo kubwa la majeraha msimu huu, huku tayari ikiwa imempoteza Khvicha Kvaratskhelia, ambaye naye alipata jeraha la goti katika mchezo dhidi ya Barcelona, Oktoba.

PSG sasa itarejea uwanjani Jumatano, ikiwa mwenyeji wa AS Roma katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii