WANANCHI WALAANI VITENDO VYA KUWATELEKEZA WATOTO ILEMELA.

Wananchi wa Mtaa wa Chamwenda, Kata ya Nyasaka, Halmashauri ya Wilaya ya Ilemela, mkoani Mwanza, wamelaani vitendo vya kutelekeza miili ya watoto wachanga, huku wakitaka hatua za kisheria zichukuliwe dhidi ya wanaojihusisha na vitendo hivyo ili kukomesha tatizo hilo katika jamii.

Wakizungumza kuhusu tukio hilo, baadhi ya wananchi, Sharif Hassan na Beatus Rajabu, wamesema vitendo hivyo vinapaswa kukomeshwa, huku wakihimiza jamii kutoa taarifa kwa viongozi na mamlaka husika kila inapobaini matukio hayo.

Wameongeza kuwa wanawake na wanaume wanapaswa kushirikiana katika malezi na uwajibikaji wa kifamilia ili kusaidia kupunguza matukio ya aina hiyo yanayozua taharuki katika jamii.

Balozi wa Shina Namba 8 katika Mtaa wa Chamwenda, Deusdedit Kabasa, ameeleza hatua zinazoendelea kuchukuliwa kufuatia tukio hilo, akisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya viongozi na wananchi katika kukabiliana na tatizo hilo.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Mtaa wa Chamwenda, Editha Leonard, amekemea vikali vitendo vya kutelekeza miili ya watoto, akiwataka wazazi kuwajibika katika malezi ya watoto wao.

Amesisitiza kuwa jamii ina wajibu wa kulinda haki na usalama wa watoto, huku akiwataka wananchi kutoa taarifa kwa viongozi wa serikali za mitaa na mamlaka husika pindi wanapobaini vitendo vya kutelekeza watoto ili hatua zinazostahili zichukuliwe

Kwa upande wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza, kupitia taarifa iliyotolewa Oktoba 29, 2026, limethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa linaendelea na uchunguzi kuhusu kupatikana kwa miili ya vichanga wawili wa jinsia ya kiume wanaodhaniwa kuwa mapacha, ambao wanakadiriwa kuwa na umri wa miezi mitano hadi sita tangu kutungwa kwa mimba.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, miili ya vichanga hao ilikutwa imetelekezwa jalalani baada ya mwanamke ambaye jina lake na makazi yake hayajafahamika kudaiwa kutoa mimba na kusababisha vichanga hao kufariki dunia. Miili hiyo imehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha Hospitali ya Rufaa ya Sekou Toure jijini Mwanza.

Aidha, Jeshi la Polisi limewataka wananchi wenye taarifa zinazoweza kusaidia uchunguzi kuzifikisha kwa mamlaka husika ili kusaidia kubaini na kumkamata mtuhumiwa wa tukio hilo.

Tukio hilo limetokea Oktoba 27, 2026, majira ya saa 12:45 jioni, katika Mtaa wa Chamwenda, Kata ya Nyasaka, Wilaya ya Ilemela.

Imeandikwa| Martin Mbilinyi

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii