SAFARI ZA MOJA KWA MOJA ZA NDEGE TANZANIA NA ANGOLA ZANUKIA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema Tanzania na Angola zimekubaliana kuimarisha ushirikiano katika sekta ya usafiri na usafirishaji, ikiwemo kuwezesha safari za moja kwa moja za anga kati ya nchi hizo mbili ili kukuza biashara, uwekezaji na utalii.

Akizungumza Ikulu jijini Dar es Salaam leo, Alhamisi, Oktoba 29, 2026, baada ya mazungumzo na Rais wa Angola, João Manuel Gonçalves Lourenço, Rais Samia amesema nchi hizo zimetia saini mkataba wa huduma za usafiri wa anga utakaowezesha kuanzishwa kwa safari za moja kwa moja.

Amesema usafiri ni miongoni mwa vikwazo vinavyoathiri ukuaji wa biashara baina ya nchi hizo, hivyo viongozi hao wamekubaliana kuimarisha ushirikiano katika sekta ya usafiri wa anga, reli na majini.

Aidha, amesema Tanzania na Angola zinaendelea kuweka mazingira bora ya kuunganisha shoroba za usafirishaji za Lobito na Dar es Salaam, hatua inayotarajiwa kuimarishwa na kukamilika kwa miradi ya ukarabati wa reli ya TAZARA na reli ya Benguela nchini Angola.

Rais Samia ameeleza kuwa kukamilika kwa miradi hiyo kutarahisisha usafirishaji wa bidhaa na kuimarisha muunganiko wa kiuchumi kati ya nchi hizo na maeneo jirani.

Vilevile, amesema Tanzania na Angola zimekubaliana kuandaa kongamano la biashara na uwekezaji litakalowakutanisha wafanyabiashara na sekta binafsi za nchi hizo ili kubaini fursa za ushirikiano na kuongeza kiwango cha biashara baina yao.

Amesisitiza kuwa hatua hizo ni sehemu ya juhudi za kuimarisha uhusiano wa kihistoria uliopo kati ya Tanzania na Angola na kuugeuza kuwa fursa halisi ya maendeleo ya kiuchumi kwa wananchi wa nchi hizo mbili.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii