Álvarez aomba radhi kwa bao

MSHAMBULIAJI wa Atlético Madrid, Julián Álvarez, ameomba radhi kwa mashabiki wa klabu hiyo kutokana na kauli zake za kutaka kuondoka na kujiunga na Barcelona wakati wa mapumziko ya Kombe la Dunia.

Álvarez ametoa kauli hiyo baada ya kufunga bao pekee lililoipa Atlético Madrid ushindi wa mabao 1-0 dhidi ya Deportivo La Coruña katika mchezo wa Ligi Kuu Hispania, LaLiga, uliochezwa juzi.

Bao hilo alilofunga dakika ya 48 lilikuwa muhimu kwa Atlético, ambayo iliendelea kujiimarisha katika mbio za ubingwa wa LaLiga, ikiwa pointi mbili nyuma ya vinara Barcelona kabla ya mchezo wa El Clásico uliotarajiwa kuchezwa jana kwenye Uwanja wa Camp Nou.

Nyota huyo wa Argentina alikumbwa na wakati mgumu baada ya kuibuka kwa taarifa za kutaka kuondoka Atlético Madrid na kujiunga na Barcelona, jambo lililozua hasira miongoni mwa mashabiki wa timu hiyo.

Akizungumza baada ya mchezo huo, Álvarez alikiri kuwa alikosea namna alivyowasilisha hisia zake kuhusu mustakabali wake na muda alioutumia kutoa kauli hizo.

“Ninataka kuwaomba radhi mashabiki wetu kwa maneno yangu wakati wa Kombe la Dunia. Ilikuwa makosa kwa namna nilivyoeleza nilichomaanisha na wakati niliouchagua kufanya hivyo,” alisema Álvarez.

Aliongeza kuwa anaelewa sababu za mashabiki kukasirika, hasa kutokana na namna walivyompokea na kumuunga mkono tangu alipojiunga na klabu hiyo.

“Ninaelewa hasira zao, hasa ukizingatia jinsi walivyonisaidia tangu nilipowasili. Wamenipa upendo mkubwa. Sasa ni wakati wa kufanya kazi na kutoa kila nilicho nacho kwa ajili ya timu,” alisema.

Kauli hiyo imekuja baada ya mshambuliaji huyo kupitia kipindi kigumu mwanzoni mwa msimu, kilichochangiwa na majeraha na kiwango kisichokuwa cha kuridhisha, hali iliyomfanya kukosolewa na baadhi ya mashabiki wa kukosolewa.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii