KOCHA Manqoba Mngqithi ameingia kwenye orodha ya kuifundisha Yanga kwa muda mfupi zaidi, ambapo miezi mitatu na siku 14 zilitosha kabisa viongozi wa klabu hiyo kumwonesha mlango wa kutokea kwa madai ya kushuka kiwango cha timu na matokeo yasiyoridhisha.
Manqoba, raia wa Afrika Kusini, ameiongoza Yanga kucheza michezo 13 chini yake katika mashindano yote, ikishinda mechi 10, sare mbili na kupoteza mmoja dhidi ya Simba mabao 2-1, Oktoba 10 mwaka huu.
Akiwa Kocha Mkuu, imeiwezesha Yanga kushinda mabao 29 na kuruhusu saba.
Anakuwa kocha wa tatu kutimuliwa kwenye Ligi Kuu msimu huu hadi sasa, wa kwanza akiwa ni Etienne Ndayiragije raia wa Burundi akiwa TRA United ambapo sasa kijiti chake kimechukuliwa na mzawa, Hemed Suleiman 'Morocco' na Juma Kaseja wa Kagera Sugar, nafasi yake sasa ikishikiliwa na Mrundi, Cedric Kaze.
Kibarua cha Manqoba kiliota nyasi rasmi juzi mara baada ya kumalizika kwa mchezo wa Ligi Kuu kati ya timu aliyokuwa akiifundisha dhidi ya TRA United kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha.
Baada ya mchezo huo kikao cha Kamati ya Utendaji ya Yanga kilifanya maamuzi ya kumpa mkono wa kwaheri kocha huyo na benchi lake lote la ufundi.
"Vile vile uongozi wa Yanga umesitisha mkataba na kocha wa viungo wa timu ya kwanza, Chyna Mokalla, na tayari mchakato wa haraka kumpata kocha mkuu mpya umeanza na unatarajiwa kukamilika hivi karibuni," ilisema taarifa ya Ofisa Mtendaji Mkuu wa klabu hiyo.
Katika kipindi chake kifupi kilichoanza Julai 10 mwaka huu, akichukua nafasi ya Pedro Gonçalves raia wa Ureno, alifanikiwa kuifikisha Yanga kwenye hatua ya makundi, Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kuifunga CFFA ya Madagascar jumla ya mabao 8-1, ikiwamo kuifunga Simba bao 1-0 katika mchezo wa Ngao ya Jamii.
Presha kwa Manqoba ilianza kabla hata ya kucheza na Simba Oktoka 10, ambapo mashabiki wengi wa timu hiyo walionekana kukerwa na kiwango duni wakidai timu haichezi soka la kuvutia.
Kipigo cha mabao 2-1 kutoka kwa Simba ni kama kidonda kilichotiwa chumvi, ingawa pamoja na kelele za mashabiki uongozi ulikuwa kimya, hadi juzi ambapo suluhu dhidi ya TRA United ilikuwa kama kibiriti kilichowashwa kwenye petroli.
Suluhu hiyo imeifanya Yanga kufikisha pointi 19 ikiendelea kuwa nafasi ya pili, ikiachwa pointi tano na Simba inayoongoza ligi kwa pointi 24.