Kwa vifo 9 na wagonjwa 76 waliorekodiwa hadi sasa, mlipuko wa dondakoo (Difteria) unaathiri maeneo 11 kati ya 14 ya Senegal, haswa eneo la Kédougou mashariki. Mamlaka za afya zinatoa wito wa kumwona daktari haraka mara tu dalili za kwanza za homa zinapoanza na kupata chanjo.
Mgonjwa wa kwanza wa dondakoo nchini Senegal aliripotiwa Julai 30 katika eneo la Kédougou. Kuwepo kwake katika upande wa mashariki wa nchi, karibu na Mali, kunafanya idhaniwe kuwa ni maambukizi ya mipakani.
Mali, Mauritania, na Guinea zote zimekuwa zikishughulika na visa vingi vya diphtheria tangu mwaka 2025, hali ambayo inaweza kuelezea kuwasili kwa ugonjwa huo nchini.
Kwa kuongezea hayo, kiwango cha chanjo nchini Senegal ni asilimia 88, ambacho ni kizuri kiasi, lakini ugonjwa huu unaoambukiza kwa urahisi unaenea zaidi miongoni mwa watoto ambao hawajachanjwa.
Kwa sababu hiyo, mamlaka za afya zinatoa wito kwa wananchi kuwa waangalifu na kumuona daktari haraka pindi wanapohisi maumivu ya koo na homa. Hii ni kwa sababu dondakoo (Difteria) hakika ni ugonjwa uanaoua, lakini pia unaweza kutibika kwa urahisi.
Hadi sasa, wagonjwa 249 wanaoshukiwa wametambuliwa. Baada ya Kédougou, Dakar na Thiès, maeneo yenye watu wengi zaidi nchini, ndiyo yaliyoathiriwa zaidi.