Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimesema hakiwezi kuingilia mihimili ya dola kwa kuwa kila mhimili una majukumu yake kwa mujibu wa katiba na sheria.
Kimesema Mahakama ni miongoni mwa mihimili inayopaswa kutekeleza majukumu yake kwa uhuru na kwa kuzingatia sheria.
Hayo yameelezwa na Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Stephen Wasira wakati akifungua mafunzo ya itikadi na uenezi kwa makada wa chama yaliyofanyika katika Chuo cha CCM, mkoani Iringa, jana.
Wasira amebainisha kwamba, kuheshimu mgawanyo wa madaraka ni sehemu muhimu ya uendeshaji wa nchi kwa misingi ya kikatiba.
“Hivyo siyo sahihi kwa chama cha siasa kuingilia utekelezaji wa majukumu ya Mahakama au mhimili mwingine unaotambulika kikatiba,” amesema.
Pia amesema kuwa chama hicho kitaendelea kuwa mfano wa demokrasia nchini, kikisisitiza kuwa misingi hiyo inaanza ndani ya chama chenyewe.
Amesema CCM imekuwa ikizingatia misingi ya demokrasia katika uendeshaji wa shughuli zake, ikiwemo katika mchakato wa uchaguzi wa viongozi wake.
“Uchaguzi unaofanyika ndani ya chama unalenga kutoa nafasi kwa wanachama kushiriki katika kuwachagua viongozi wanaowataka kwa mujibu wa taratibu zilizowekwa.
“Hatua hiyo ni sehemu ya kuhakikisha misingi ya demokrasia inaendelea kuimarika ndani ya chama,” amesema Wasira.
Pia amevitaka vyama vingine vya siasa nchini kuiga mfano huo kwa kuhakikisha vinazingatia demokrasia katika shughuli zake na uchaguzi wa viongozi wao.
Mkongwe huyo wa siasa nchini ameongeza kuwa, demokrasia ni muhimu katika kujenga vyama imara, vinavyoweza kuwajibika kwa wanachama na wananchi kwa ujumla.