Serikali imewataka wananchi kuwa makini katika ununuzi na matumizi ya majokofu na viyoyozi, ikiwemo kuepuka vifaa vilivyotumika (mitumba) vinavyotumia gesi zinazoharibu tabaka la ozoni na kuchangia ongezeko la joto duniani.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhandisi Hamad Yussuf Masauni, ametoa kauli hiyo jana jijini Dar es Salaam akizungumza na waandishi wa habari kuelekea siku ya Kimataifa ya Hifadhi ya tabaka la Ozoni Septemba 16.
Amesema wananchi wanapaswa kununua vifaa vilivyo na nembo rasmi zinazoonesha “Ozone Friendly” au “Low Global Warming Potential”, ili kupunguza madhara kwa mazingira.
Pia amewataka wananchi kuepuka kutupa ovyo majokofu ya zamani na vifaa vya kuzimia moto vyenye kemikali zinazoweza kuharibu tabaka la ozoni au kuchangia ongezeko la joto duniani.
“Tabaka la ozoni lina jukumu muhimu la kuchuja sehemu kubwa ya mionzi ya jua ili isifike moja kwa moja kwenye uso wa dunia. Uharibifu wake unaweza kuongeza hatari ya magonjwa kama saratani ya ngozi na mtoto wa jicho, pamoja na kuathiri ukuaji wa mimea,” amesema Mhandisi Masauni.
Pia Katibu Mkuu wa Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Dk. Richard Muyungi, amesema nchi iko tayari kushirikiana na nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa katika juhudi za kulinda tabaka la ozoni na kukabiliana na changamoto za mazingira na mabadiliko ya tabianchi.