Shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula WFP, limesema litazimika kusitisha utoaji wa msaada wa chakula kwa raia wa Sudan Kusini wapatao Milioni mbili, hivi karibuni kwa sababu ya uhaba wa fedha.
WFP imetoa onyo hili, katika kipindi ambacho watu zaidi ya Milioni 7.8 wanapokabiliwa na changamoto ya kupata chakula cha uhakika nchini Sudan Kusini.
Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika hilo Matthew Hollingworth, amesema iwapo fedha hazitopatikana kwa wakati, idadi ya watu wanapokea msaada wa chakula kila siku, itapungua kwa kiasi kikubwa kufikia mwisho wa mwezi wa Septemba.
Ripoti hii inakuja, wakati huu watoto Milioni 2.2 wakiwemo wanawake wajawazito 1.2 wakihitaji lishe bora kwa ajili ya kuimarisha afya zao.
Aidha, WFP inasisitiza kuwa inahitaji Dola Milioni 86 haraka na Dola nyingine Milioni 416 ndani ya miezi sita zijazo, ili kuendelea kuwasaidia raia wa Sudan Kusini kupata chakula cha uhakika.