Polisi waanza operesheni kukamata bodaboda, bajaji wanaovunja sheria

Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani limeanza leo, Septemba 29, 2026, operesheni maalumu ya kuwabana waendesha pikipiki (bodaboda) na bajaj wanaokiuka sheria na kanuni za usalama barabarani.

Operesheni hiyo inatekelezwa nchini kote kwa lengo la kuongeza utii wa sheria za usalama barabarani na kupunguza makosa yanayoweza kusababisha ajali, majeruhi na vifo.

Miongoni mwa makosa yanayolengwa katika operesheni hiyo ni kutovaa kofia ngumu (helmet), kubeba abiria zaidi ya idadi inayoruhusiwa kisheria, pamoja na kutofuata utaratibu unaotakiwa wa kukaa ndani ya bajaji.

Aidha, polisi watachukua hatua dhidi ya makosa mengine yanayokiuka sheria na kanuni za usalama barabarani.
Kamanda wa Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani Tanzania, SACP William Mkonda, ameyaeleza hayo wakati akizungumza na viongozi wa vyama vya madereva wa pikipiki na bajaji pamoja na viongozi wa wilaya za Mkoa wa Dar es Salaam.

SACP Mkonda amewataka madereva hao kuzingatia sheria na kanuni za usalama barabarani ili kujikinga wao wenyewe, abiria na watumiaji wengine wa barabara dhidi ya madhara yanayoweza kusababishwa na uzembe au ukiukaji wa sheria

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii