Rais wa Marekani Donald Trump, amekanusha ripoti za kupunguza baadhi ya vikwazo dhidi ya Iran, na kuagiza kuachiwa kwa fedha zinazozuiwa, wakati huu mkataba wa kumaliza vita ukiwa bado haujapatikana.
Trump, amesema taarifa zilizotolewa na Shirika la Habari la Axios kuhusu hatua hiyo, ni za uongo.
Kupitia ukurasa wake wa kijamii wa Truth, Trump amesisitiza kuwa, hajafanya lolote kwa Iran.
Ripoti hiyo ya Shirika la Axios, imeeleza kuwa Trump, alikuwa tayari kupunguza au kuondoa vikwazo dhidi ya Iran, kama njia ya kuishawishi kuachana kabisa na mradi wake wa Nyuklia.
Haya yamejiri, huku Waziri wa Mambo ya nje wa Iran Abbas Araghchi, akikutana na wasuluhishi wa mzozo huu kutoka Qatar, jijini New York.
Wiki iliyopita, maafisa wa Marekani na Iran, walikutana pembezoni mwa mkutano mkuu wa Umoja wa Mataifa wakati huu jitihada zikiendelea kujaribu kutafuta mkataba wa kudumu.
Jumamosi iliyopita, rais Trump alikataa mapendekezo ya Iran kuhusu kufunguliwa kwa mlango Bahari wa Hormuz.