Jeshi la serikali ladai kuchukua udhibiti wa Mji wa Alamata

Jeshi la Ethiopia na vikosi vinavyounga mkono serikali vimedai kuuteka mji wa kimkakati wa Alamata, kusini mwa mji mkuu wa Tigray, Mekelle. Hatua hiyo imebadili mwelekeo wa mapigano, baada ya mashambulizi kuanzishwa na upande wa upinzani katika eneo hilo wiki iliyopita.

Video iliyochapishwa kwenye ukurasa wa Facebook wa Tigray Peace Force, kundi linalounga mkono serikali, iliwaonyesha wanajeshi wakitembea katika mitaa ya Alamata huku wakipeperusha bendera ya Ethiopia.

Hata hivyo, jeshi la Ethiopia pamoja na wapiganaji wa Tigray People’s Liberation Front, TPLF, hawajathibitisha taarifa hizo. Vyanzo vya kidiplomasia katika eneo hilo, hata hivyo, viliripoti kuwa mji wa Alamata umetwaliwa na vikosi vinavyoiunga mkono serikali.

Kutekwa kwa Alamata ni mafanikio muhimu kwa vikosi vya serikali, ambavyo sasa vinasonga mbele kuelekea Mekelle, makao makuu ya eneo la Tigray, yaliyoko takriban kilomita 120 kaskazini mwa Alamata.

Mapigano hayo, yaliyoanza Jumatano wiki iliyopita katika eneo la Tigray na maeneo jirani ya Amhara na Afar, yameibua wasiwasi kuhusu kuvunjika kwa makubaliano ya amani yaliyotiwa saini jijini Pretoria miaka minne iliyopita.

Makubaliano hayo yalihitimisha vita vya Tigray vilivyodumu kwa miaka miwili na kusababisha vifo vya mamia ya maelfu ya watu.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii