Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), imesema watu 8,067 wamethibitishwa kuambukizwa ebola na 3,901 wamefariki.
Kwa mujibu wa serikali, mlipuko huo umeenea katika majimbo saba nchini humo.
Takwimu zinaonesha kwamba hii ndiyo mara ya kwanza kwa idadi ya maambukizi kuvuka 8,000 tangu mlipuko huu ulipogunduliwa Mei, 2026.
Shirika la Afya Duniani (WHO), linasema maeneo mawili zaidi ya huduma za afya yameathirika, huku wataalamu wakionya kwamba wagonjwa wengi wapya wanagunduliwa nje ya mfumo wa kufuatilia watu waliokutana na waathirika.
Mlipuko huo unaosababishwa na aina ya virusi vya ebola iitwayo Bundibugyo, tayari ni mkubwa na wenye vifo vingi zaidi katika historia ya DRC. Duniani, ni mlipuko wa pili kwa ukubwa baada ya ule ulioikumba kanda ya Afrika Magharibi kati ya mwaka 2014 na 2016.
WHO limesema eneo la Bulu katika jimbo la Sud Ubangi na eneo la Dungu katika jimbo la Haut-Uele, karibu na mpaka wa Sudan Kusini, yameathirika.
Bulu na Dungu ndiyo maeneo mawili yaliyotambuliwa hivi karibuni.