Italia na Ujerumani zatafuta mwafaka kuhusu uhamiaji

Waziri wa Mambo ya Nje wa Italia Antonio Tajani amesema Ujerumani na Italia zinataka kuimarisha ushirikiano katika kushughulikia suala la uhamiaji kufuatia tofauti kuhusu namna ya kushughulikia suala la wahamiaji.

Baada ya mazungumzo kwa njia ya simu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Johann Wadephul, Tajani amesema kuwa suala la uhamiaji limekuwa ajenda kuu ya mazungumzo kati ya Rome na Berlin.

Mwanadiplomasia huyo aliandika katika mtandao wa kijamii wa X kwamba, pande zote mbili zimekubaliana kuhusu "umuhimu wa kuhakikisha ulinzi wa hali ya juu zaidi wa mipaka ya nje ya Ulaya."

Hata hivyo, Tajani hakuzungumzia tofauti zilizopo kati ya nchi hizo kuhusu iwapo Italia inapaswa kuwapokea tena waomba hifadhi walioingia katika Umoja wa Ulaya kupitia Italia kabla ya kuelekea Ujerumani.

Ujerumani inataka kuwarejesha wahamiaji hao nchini Italia kwa mujibu wa sheria zilizopo za Umoja wa Ulaya kuhusu uhifadhi, lakini serikali ya mrengo wa kulia inayoongozwa na Waziri Mkuu Giorgia Meloni hadi sasa imekataa kuwapokea tena.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii