Rais wa Marekani Donald Trump ametishia kuishambulia Oman ikiwa nchi hiyo itazuia juhudi za kutatua mgogoro unaohusu Mlango Bahari wa Hormuz.
Trump ameitoa kauli hiyo Jumatatu wakati ambapo mazungumzo kati ya Marekani na Iran yakiendelea kukwama, huku Oman na Iran zikijadiliana kuhusu uwezekano wa kurejesha shughuli za kawaida za usafirishaji wa meli katika njia hiyo muhimu ya usafirishaji wa mafuta na gesi duniani.
Mvutano kuhusu udhibiti wa Mlango wa Hormuz umechangia kupanda kwa bei za mafuta na kuongeza shinikizo kwa Trump kumaliza vita hivyo, hasa wakati huu Marekani ikielekea katika uchaguzi wa katikati ya muhula utakaofanyika mwezi Novemba.
Hayo yakiarifiwa, Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdoğan amezungumza kwa njia ya simu na rais Trump na akamtaka kuendeleza mazungumzo na Iran ili kupunguza mvutano, huku akisisitiza kuwa Uturuki iko tayari kusaidia juhudi za kutafuta amani na suluhisho la kidiplomasia.