Mamia ya raia wa Tunisia wameandamana katika mji mkuu, Tunis, wakilalamikia ukosefu wa maji, umeme na kupanda kwa gharama za maisha wakati nchi hiyo ikikabiliwa na wimbi la joto kali.
Waandamanaji, wakiongozwa na muungano mpya wa upinzani Nafas, wanamtaka Rais Kais Saied aondoke madarakani wakisema serikali imeshindwa kutoa huduma za msingi.
Mgao wa umeme umeathiri vituo vya kusukuma maji, na kuzidisha tatizo la upatikanaji wa maji ya kunywa. Baadhi ya maduka yameripotiwa kuishiwa maji ya chupa kutokana na changamoto za uzalishaji.
Waandamanaji pia wanapinga kile wanachokiita kushindwa kwa serikali kushughulikia mahitaji ya wananchi na kudorora kwa uhuru wa kisiasa na mafanikio ya mapinduzi ya 2011 yanaporomoka.
Rais Saied ameimarisha mamlaka yake tangu mwaka 2021, hatua ambayo wakosoaji wanasema imeongeza vikwazo dhidi ya vyombo vya habari, mashirika ya kiraia na wapinzani wa kisiasa.
Kauli za kumtaka Rais Saied kuondoka madarakani zimezidi kusikika katika maandamano ya hivi karibuni.