Nchini Nigeria, watu wenye silaha wamewauwa watu zaidi ya 60 wanaolinda usalama katika kijiji chao wilayani Zuru katika jimbo la Kebbi, Kaskazini Magharibi mwa nchi hiyo baada makabiliano makali hapo jana.
Zaidi ya makundi mia moja ya wahalifu yanaendesha shughuli zao kati ya majimbo ya Zamfara, Niger, Sokoto na Kebbi, ambako yanazidisha ukatili mbaya, katika hali ambayo vikosi vya usalama vinaonekana kutokuwa na nguvu.
Walikuwa mstari wa mbele, wakikabiliana na makundi yenye silaha ambayo yamekuwa yakitekeleza uhalifu na mashambulizi mbalimbali kaskazini magharibi mwa Nigeria kwa miezi kadhaa. Katika Jimbo la Kebbi, wanamgambo wa kujilinda wa "Yan Sa Kai", kundi la wapiganaji wa kujitolea kutoka eneo la Sakaba, walipanga kushambulia kundi la majambazi Jumapili Machi 6 usiku. Inaonekana wanamgambo hao walikuwa wameenda kuwasaka watu wenye silaha ambao walikuwa wamevamia vijiji kadhaa katika wilaya ya Sakaba.
Mmoja wa viongozi wa wanamgambo hao, Usman Sani, mwanajeshi wa zamani aliyehojiwa na shirika la habari la Reuters, amesema kwamba wanachama wa genge hilo, walioonya juu ya shambulio hilo, waliandaa shambulio la kuvizia, wakitumia fursa ya msitu ambao wanaufahamu vyema. Baada ya kuficha pikipiki zao, waliwazunguka wapiganaji wa kujitolea kabla ya kufyatua risasi kutoka pande kadhaa.
Mbali na mauaji hayo, watu hao wenye silaha, waliiba mifugo.
Rais
Muhammadu Buhari ameelaani mauaji hayo katika nchi hiyo ambayo
imeendelea kushuhudia ukosefu wa usalama kutokana na kuwepo kwa kundi la
Boko Haram na makundi yenye silaha.