Mahakama nchini Kenya imemkuta na hatia gavana wa zamani wa kaunti ya Migori, Okoth Obado, katika kesi ya mauaji ya mwanafunzi wa chuo kikuu cha Rongo, Sharon Otieno ambaye aliuawa akiwa mjamzito.
Hukumu hiyo ilitolewa baada ya kesi ya karibu miezi saba, ambapo pia aliyekuwa msaidizi wa kibinafsi wa Obado, Michael Oyamo na aliyekuwa karani wa Kaunti ya Migori Caspal Obiero pia walipatikana na hatia ya kumuua mwanafunzi huyo.
Kulingana na mahakama kuu ya milimani, jijini Nairobi, upande wa mashtaka ulitoa ushahidi tosha kuwawatatu hao walishirikiana kupanga na kutekeleza mauaji ya Sharon, ambaye wakati wa kifo chake alikuwa na ujauzito wa wiki 28.
Aidha mahakama ilisema kuwa mwathiriwa alikuwa akimshinikiza Obado kukubali hadharani kuwa mimba aliokuwa ameibeba ni yake, na hivyo mahakama hiyo kubainisha kuwa Obado ndiye aliyekuwa na sababu ya kutaka Sharon auawe kwa usaidizi wa wawili hao.
Hukumu hii inamanisha kuwa watatu hao watasubiri adhabu baada ya kuhitimishwa kwa kesi hiyo, huku pia mahaka hiyo ikifuta dhamna yao na kutakiwa kurejeshwa rumande hadi Agosti 18 kabla ya hukumu ya mwisho.