Wagombea sita wanaowania nafasi ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa wameweka msisitizo mkubwa juu ya kurejesha imani kwa taasisi hiyo, ambayo kwa sasa inakabiliwa na changamoto kubwa.
Wagombea hapo waliyasema hayo wakati wa mdahalo uliofanyika jana kwenye ukumbi mkubwa wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa wiki moja kabla ya kuanza rasmi kwa mchakato wa kumchagua Katibu Mkuu mpya.
Michelle Bachelet wa Chile, Maria Fernanda Espinosa wa Ecuador, Rafael Grossi wa Argentina, Rebeca Grynspan wa Costa Rica, Carolyn Rodrigues-Birkett wa Guyana na Macky Sall wa Senegal wanawania kumrithi Mreno Antonio Guterres anayemaliza muda wake Disemba 31.
Wagombea hao walijibu maswali kwa karibu saa mbili kutoka kwa wanadiplomasia, wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa na wawakilishi wa mashirika ya kiraia.
Kila mgombea alieleza sababu zinazomfanya awe chaguo bora, wakisisitiza uwezo wao wa kukabiliana na kipindi kigumu cha migogoro mingi duniani.
Pia walitaja uzoefu wao katika ngazi za kitaifa au kimataifa na kueleza uwezo wao wa kuzungumza na pande zinazohusika katika migogoro.