NAIBU WAZIRI WA NISHATI AFUNGUA MKUTANO WA WADAU WA NISHATI SAFI JIJINI ARUSHA

Naibu Waziri wa Nishati, Salome Makamba, amesema Tanzania imepata mafanikio makubwa katika utekelezaji wa ajenda ya nishati safi ya kupikia, ambapo kiwango cha matumizi kimeongezeka kutoka asilimia 6.9 mwaka 2021 hadi asilimia 28.6 mwaka 2025.
Ameyasema hayo jijini Arusha wakati akifungua mkutano uliolenga kujadili  fursa, changamoto na mbinu za kuongeza matumizi ya teknolojia za kupikia ambazo ni salama kwa afya na mazingira.
“Watanzania wengi zaidi wanapata huduma za nishati safi ya kupikia zimepewa msukumo mpya baada ya wadau kutoka sekta ya umma, binafsi na mashirika ya maendeleo kukutana jijini Arusha kujadili mikakati ya kuharakisha upatikanaji wa nishati hiyo nchini. “amesema Makamba .
Amesema ongezeko hilo linaonesha namna juhudi za Serikali na ushirikiano wa wadau mbalimbali zinavyoendelea kuleta matokeo chanya katika kuboresha maisha ya wananchi.
Makamba ameongeza  kuwa Serikali imeweka lengo la kuhakikisha asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034 kupitia utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Nishati Safi ya Kupikia wa mwaka 2024–2034.
 “mkakati huo umejikita katika kuongeza upatikanaji wa teknolojia nafuu za kupikia, kuimarisha ushiriki wa sekta binafsi na kuhamasisha wananchi kubadili matumizi ya nishati za jadi zinazochangia uharibifu wa mazingira.”amesema Makamba .
Amefafanua  kuwa, mafanikio yaliyofikiwa hadi sasa yamechangiwa na utekelezaji wa miradi mbalimbali ikiwemo usambazaji wa mitungi 452,445 ya gesi ya LPG, majiko banifu zaidi ya 200,000 pamoja na mradi wa CookFund unaofadhiliwa na Umoja wa Ulaya kupitia UNCDF ambapo miradi hiyo imewezesha mamia ya maelfu ya wananchi katika mikoa mbalimbali kupata huduma za nishati safi na salama ya kupikia.
Katika mkutano huo, Balozi wa Umoja wa Ulaya nchini Tanzania, Christine Grau, ametangaza kuwa EU imetenga euro milioni 30, sawa na zaidi ya shilingi bilioni 92, kwa ajili ya kusaidia upanuzi wa matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini.
Amesema uwekezaji huo unalenga kuimarisha masoko ya nishati endelevu, kuvutia uwekezaji wa sekta binafsi na kuongeza upatikanaji wa huduma kwa wananchi wa maeneo ya mijini na vijijini.
Grau alisema ufadhili huo ni sehemu ya mkakati wa Global Gateway unaolenga kuharakisha maendeleo endelevu kupitia uwekezaji katika sekta muhimu za kiuchumi.
 Amesisitiza kuwa matumizi ya nishati safi ya kupikia yana mchango mkubwa katika kulinda mazingira, kupunguza ukataji wa miti na kuboresha afya za wanawake na watoto ambao mara nyingi huathiriwa na moshi unaotokana na matumizi ya nishati za jadi.
Nao baadhi ya  wadau walioshiriki mkutano huo,wamesema kuwa , ushirikiano kati ya Serikali, washirika wa maendeleo na sekta binafsi utaendelea kuwa nguzo muhimu katika kufanikisha ajenda ya nishati safi ya kupikia nchini.
 Walisema hatua zinazochukuliwa kwa sasa zinaipa Tanzania nafasi nzuri ya kufikia malengo yake ya mwaka 2034 huku zikichangia ustawi wa wananchi, uhifadhi wa mazingira na maendeleo ya uchumi wa taifa kwa ujumla.

10YrsJembefm  #Familiamoja #AhsantekwaTime

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii