Umoja wa Mataifa unasema dunia inaonekana kuisahau nchi ya Sudan, ambayo imeendelea kuwa kwenye vita kwa karibu miaka mitatu sasa kati ya wanajeshi na wanamgambo wa RSF.
Mjumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Denise Brown, amesema kuendelea kwa vita kunaonesha kuwa, hakuna anayejali kuhusu mauaji na visa vingine vya ukiukwaji wa haki za binadamu vinavyoendelea.
Mbali na mauaji, mjumbe huyo amesema matukio ya ubakaji wa wanawake na wasichana, watu kuyakimbia makwao ni mambo ambayo raia wa Sudan wanaendelea kupitia huku dunia ikiendelea kutazama.
Mzozo wa Sudan ulianza karibu miaka mitatu iliyopita kati ya wanajeshi na wanamgambo wa RSF wanaopambania uongozi wa nchi hiyo, umesababisha vifo vya maelfu ya watu na wengine zaidi ya Milioni 11 kuyakimbia makaazi yao.
Umoja wa Mataifa unaomba msaada wa Dola Bilioni 2.9 mwaka huu kuwasaidia raia wa Sudan waliothiriwa na vita, lakini ni asilimia 16 tu msaada ndio uliopatikana mpaka sasa hivi.