Rais wa Iran Alaani Kauli za Trump Dhidi ya Papa Leo XIV

Rais wa Iran Masoud Pezeshkian amejiingiza katika mjadala unaoendelea kati ya Rais wa Marekani Donald Trump na Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani Pope Leo XIV kwa kulaani vikali kauli za Trump dhidi ya Papa.

Kupitia ujumbe wake kwenye mitandao ya kijamii Pezeshkian alisema analaani kile alichokiita “matusi” dhidi ya Papa, akisisitiza kuwa kauli hizo hazikubaliki kwa watu wanaojali amani na heshima.

“Utakatifu wako Papa Leo XIV ninalaani matusi dhidi yako kwa niaba ya taifa kubwa la Iran na natangaza kuwa kudhalilisha mafundisho ya amani na undugu si jambo linalokubalika kwa mtu yeyote mwenye uhuru,” aliandika Pezeshkian.

Kauli hiyo imekuja baada ya Trump kumkosoa Papa Leo XIV kwa misimamo yake kuhusu sera za kimataifa, akimtaja kuwa “hafai katika masuala ya sera za nje” miongoni mwa shutuma nyingine.

Kwa upande wake Papa Leo XIV alizungumza kwa kifupi na waandishi wa habari akieleza kuwa haogopi utawala wa Trump huku akiepuka kuingia moja kwa moja katika mabishano hayo.

Hata hivyo Papa alitoa kauli ya kejeli kwa njia ya mafumbo aliporejea jina la mtandao wa kijamii wa Trump, Truth Social.

“Ni jambo la kushangaza hata jina la mtandao wenyewe linaeleza mengi. Sitosema zaidi,” alisema Papa.

Mvutano huo unaendelea kuvuta hisia za kimataifa huku ukihusisha viongozi wa kisiasa na kidini na kuibua mjadala mpana kuhusu mipaka ya heshima, uhuru wa kujieleza na nafasi ya dini katika siasa za dunia.

10YrsJembefm  #Familiamoja #AhsantekwaTime

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii