Iran yasema haina mpango wa kushiriki awamu ya pili ya mazungumzo

Iran inasema haina mpango wa kutuma wajumbe wake nchini Pakistan kushiriki kwenye mazungumzo mapya na Marekani, hatua ya Tehran ikija wakati huu mkataba wa kusitisha vita ukielekea kukamilika.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya nje wa Iran, Esmaeil Baghaei, amesema Marekani imekiuka mkataba wa usitishwaji vita kuanzia mwnazo, hasa baada ya kuzuia meli za Iran kupita katika mlango wa Bahari ya Hormuz kuanzia Aprili 13.

Kauli hii ya Iran inakuja huku rais Donald Trump akisema, ujumbe wa Marekani ukiongozwa na Makamu wake by JD Vance, unaelekea  jijini Islamabad kwa ajili ya mazungumzo mpaya.

Hali imeendelea kuwa mbaya baada ya jeshi la Marekani, usiku wa kuamkia Jumatatu, kukamata meli ya Iran iliyokuwa na kontena ya mizigo, kitendo ambacho Tehran inasema Washington, inakiuka mkataba wa kusitisha vita na sheria za Kimataifa.

Licha ya msimamo huu wa Iran, Pakistan inaendelea kusisitiza kuwa bado inapambana kuzileta pamoja pande hizo mbili kwenye meza ya mazungumzo ili kupata suluhu ya kudumu kuhusu vita ambavyo vilianza mwezi Februari.

Katika hatua nyingine nchini Lebanon, mkataba wa siku 10 wa usitishwaji vita kati ya Lebanon na Israeli unaendelea kutekelezwa vema, huku maelfu ya watu waliokuwa wameyakimbia makaazi yao Kusini mwa nchi hiyo, wakianza kurejea nyumbani.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii