Maandamano ya kupinga kupanda kwa bei ya mafuta yatarajiwa Kenya

Nchini Kenya hivi leo kunatarajiwa kushuhudiwa maandamano ya kupinga kupanda kwa bei ya mafuta.

Maandamano hayo yanatarajiwa kuongozwa na vijana wa Gen Z, wanaharakati pamoja na Wakenya wengine wanaoituhumu serikali kushindwa kuwakinga dhidi ya makali yanayotokana na kupanda kwa bei ya mafuta.

Tangu kutangazwa kwa bei mpya wiki iliopita na licha ya juhudi za serikali kuondoa ushuru wa thamani kwenye mafuta kwa shilingi 9, baadhi ya Wakenya kwenye mitandao ya kijamii wamekuwa wakitoa wito kwa wenzao kujitokeza kulalamikia ongezeko hilo.

Wanaopanga kuandamana wanasema kupanda kwa bei ya mafuta kumewaongezea mzigo wa gharama za maisha.

Ikumbukwe kuwa mwaka wa 2024, vijana wa Gen Z walishirki maandamano makubwa ya kupinga muswada tata wa fedha, maandamano ambayo kwa sehemu kubwa yalipangwa kupitia mitandao ya kijamii.

Kwa sasa lita ya petroli inauzwa kwa shilling 197.60 za Kenya wakati dieseli ikiuzwa kwa shilingi 196.63 na mafuta taa yakiuzwa kwa shilingi 152.78.

Hivi leo jeshi la polisi lilionya kuwachukulia hatua waandamanaji ambao hawajatoa taarifa, onyo linaloibua wasiwasi wa kutokea vurugu ikiwa raia watajitokeza.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii