Chad itatuma wanajeshi elfu 1 na 500 nchini Haiti ikiwa ni sehemu ya kikosi cha kimataifa kinachoungwa mkono na umoja wa Mataifa kusaidia kukabiliana na makundi ya majambazi kwenye taifa hilo, utawala wa Djamena umethibitisha.
Kwa mujibu wa rais wa Chad, Mahamat Idriss Deby Itno, nchi yake itachangia wanajeshi 750 kutoka kada mbalimbali za usalama, wakati huu tayari ikiwa imeshatuma askari wake 400.
Katika taarifa yake kwa Bunge rais Mahamat, aliwakumbusha raia na wanasiasa kuhusu mchango wa vikosi vya nchi yake katika jukumu la kulinda, akitolea mfano mafanikio ya operesheni dhidi ya makundi ya kijihadi kama Boko Haram na ushiriki wao kwenye jumuiya ya G5 Sahel.
Umoja wa Mataifa unasema makundi yenye silaha nchini Haiti yanadhibiti karibu nusu ya maeneo ya mji mkuu Port-au-Prince na mwaka jana yaliongeza wigo hadi kwenye miji jirani na kuendelea kuzorotesha hali ya usalama kwenye moja ya taifa masikini zaidi kwenye ukanda wa Amerika.
Vikosi hivi vya kulinda amani ambavyo ni vyakujitolea vinalenga kuwa na wanausalama zaidi ya elfu 5, na vilizinduliwa mwaka 2023, wanajeshi wa Chad wakienda kuchukua nafasi ya vikosi vya Kenya ambavyo vimemaliza muda wake.