Waziri Mkuu, Mwigulu Nchemba amesema Rais Samia Suluhu Hassan ameagiza fedha zilizokuwa zimetengwa kwa ajili ya maadhimisho ya miaka 62 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar zielekezwe kwenye ukarabati wa miundombinu ya barabara iliyoharibiwa na mvua zinazoendelea kunyesha nchini.
Uamuzi huo unakuja wakati mvua zimeleta uharibifu mkubwa wa barabara na madaraja katika maeneo mbalimbali, hali inayosababisha usumbufu kwa wananchi.
Akizungumza hii leo Aprili 20, 2026, jijini Dodoma, Waziri Mkuu amesema pamoja na mabadiliko hayo ya matumizi ya fedha, maadhimisho ya Muungano yatafanyika katika ngazi ya mikoa, yakihusisha viongozi kushiriki katika uzinduzi wa miradi na uwekaji wa mawe ya msingi.
Aidha, ameagiza majengo yote ya Serikali Tanzania Bara yapambwe kwa rangi za bendera ya Taifa kuanzia Aprili 20 hadi Aprili 26, 2026, ikiwa ni pamoja na kuweka picha za waasisi wa muungano na rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Hata hivyo kwa upande wa Zanzibar, amesema majengo yapambwe kwa kuzingatia rangi sahihi za bendera ya Taifa pamoja na kuweka picha za waasisi wa muungano, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.
10YrsJembefm #Familiamoja #AhsantekwaTime