Kwa sasa Tehran haijapanga kushiriki katika mazungumzo mapya na Marekani, vyombo vya habari vya serikali ya Iran vimeripoti siku ya Jumapili jioni, huku jeshi lake likiishutumu Marekani kwa kukiuka makubaliano dhaifu ya kusitisha mapigano kati ya nchi hizo mbili, saa chache baada ya Donald Trump kusema amewatuma wapatanishi kwenda Islamabad.
Rais Donald Trump alitangaza siku ya Jumapili kwamba meli ya mizigo ya Iran ambayo ilijaribu kuvuka kizuizi kilichowekwa na Marekani karibu na Mlango-Bahari wa Hormuz imekamatwa. "Tuna uangalizi kamili wa meli yao, na tunaona kilichomo ndani yake!" Trump aliandika kwenye mtandao wake kijamii wa Truth Social.
Jeshi la Iran lilisema meli hiyo ilikuwa ikisafiri kutoka China. "Tunaonya kwamba vikosi vya jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran hivi karibuni vitajibu na kulipiza kisasi dhidi ya uharamia huu wa kijeshi unaofanywa na jeshi la Marekani," vyombo vya habari vya serikali vimemnukuu msemaji wa jeshi la Iran.
Tukio hilo la siku ya Jumapili lilizua uwezekano kwamba usitishaji mapigano unaweza kushindwa kabla ya wapatanishi kuweza kukutana tena nchini Pakistan.
Marekani ilisema inatuma ujumbe kwenda Pakistan siku ya Jumatatu kwa ajili ya mazungumzo mengine yanayowezekana yenye lengo la kukomesha vita vya Marekani na Israel nchini Iran. Lakini taarifa kutoka kwa vyombo vya habari vya serikali ya Iran kwamba "kwa sasa hakuna mpango wa kushiriki katika duru inayofuata," ilionekana kuhatarisha rduru hii mpya ya mazungumzo kabla hata hayajaanza.
Kurudi kwa ujumbe wa Marekani kwenda Islamabad, ukiongozwa na makamu wa rais, JD Vance, pamoja na mjumbe maalum wa Trump, Steve Witkoff, na mkwewe, Jared Kushner, kunakuja baada ya Iran siku ya Jumamosi kuweka tena vikwazo vikali kwenye usafirishaji wa meli za kibiashara katika Mlango-Bahari wa Hormuz, ikibadilisha makubaliano yaliyofanywa saa chache kabla ya kufungua tena njia hii ya majini ya kimkakati, kuhusu kukataa kwa Marekani kuondoa kizuizi chake cha majini.
"Iran ilisema kwamba kutokuwepo kwake katika duru ya pili ya mazungumzo kulitokana na kile ilichokiita madai mengi ya Washington, matarajio yasiyo ya kweli, mabadiliko ya mara kwa mara katika msimamo, migongano ya mara kwa mara, na kuendelea kwa kizuizi cha majini, ambacho inakiona kama uvunjaji wa usitishaji mapigano," shirika la habari la serikali ya Iran IRNA limeandika.
Vita hivyo, vinavyoingia katika wiki yake ya nane, vimewaua maelfu nchini Iran na Lebanon na kusababisha bei ya mafuta kupanda kwa sababu ya kufungwa kwa njia ya bahari.
10YrsJembefm #Familiamoja #AhsantekwaTime