Zaidi ya watu 70 hawajulikani walipo baada ya boti yao kuzama katika Bahari ya Mediterania

Zaidi ya watu 70 hawajulikani walipo baada ya boti ya wahamiaji kuzama katika Bahari ya Mediterania ya Kati, na kusababisha vifo vya watu wawili, mashirika yasiyo ya kiserikali ya Mediterranea Saving Humans na Sea-Watch yameripoti siku ya Jumapili, Aprili 5, kwenye mttandao wa kijamii wa X.

Janga jingine lilitokea katika Bahari ya Mediterania mnamo Aprili 5 kwa kuzama kwa boti ya wahamiaji iliyoondoka Jumamosi alasiri kutoka Tajoura, kaskazini mwa Libya. Ndani ya boti hiyo kulikuwa na takriban wanawake, wanaume, na watoto 105 wenye asili ya BangladeshMisri, na Pakistan, kulingana na Mediterranea Saving Humans. "Tukio la kusikitisha kwa siku ya Pasaka. Manusura thelathini na wawili, miili miwili iliyopolewa, zaidi ya wahamiaji 70 ambao hawajulikani walipo," shirika hilo lisilo la kiserikali limeandika kwenye mtandao wa kijamiii wa X, likibainisha kuwa boti hiyo iliyotengenezwa kwa mbao ilizama katika eneo la utafutaji na uokoaji linalodhibitiwa na mamlaka ya Libya.

Kulingana na Sea-Watch, manusura 32 - wanaume 31 na mtoto mmoja, anaelezea mwandishi wetu huko RomaAnne Le Nir - waliokolewa na meli mbili za biashara na kutua Jumapili asubuhi katika kisiwa cha Lampedusa cha Italia. Video iliyochapishwa mtandaoni na shirika lisilo la kiserikali, na inaonekana kupigwa picha kutoka kwa ndege ya uchunguzi ya Sea-Bird 2, inaonyesha wanaume wakishikilia sehemu ya juu ya boti iliyozama, wakielea baharini, kabla ya kukaribiwa na meli ya biashara.

"Tunaungana kwa huzuni huu na familia wahanga hao, na wapendwa wao. Ajali hii ya hivi karibuni ya boti ya wahamiaji si ajali mbaya, bali ni matokeo ya sera za serikali ya Ulaya zinazokataa kufungua njia salama na za kisheria," imeandika Mediterranea Saving Humans.

Lampedusa ni sehemu ambapo wahamiaji wengi wanaovuka Mediterania kutoka Afrika Kaskazini wanafikia. Wengi wanaangamia wakijaribu safari hii hatari. Tangu mwanzoni mwa mwaka 2026, wahamiaji 683 wamefariki au kutoweka katika Mediterania ya kati, kulingana na Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM). Kulingana na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Italia, wahamiaji 6,175 walifika kwenye mwambao wa Italia wakati huo huo, kulingana na takwimu za hivi karibuni kutoka Aprili 3.

10YrsJembefm  #Familiamoja #AhsantekwaTime

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii