Trump Atangaza Kuishambulia Iran Kwa Nguvu Kubwa Kabla ya Kumaliza Vita Ndani ya Wiki 2–3

Rais wa Marekani Donald Trump amesema kuwa vita kati ya Marekani na Iran vinatarajiwa kumalizika hivi karibuni licha ya kuonya kuwa mashambulizi makubwa zaidi bado yanakuja ndani ya wiki chache zijazo.

Akihutubia taifa kupitia hotuba ya moja kwa moja usiku wa kuamkia leo Aprili 2, 2026  Trump alisema operesheni ya kijeshi dhidi ya Iran, ambayo sasa imeingia mwezi wake wa pili, inaendelea vizuri na inalenga kulinda usalama wa Marekani pamoja na dunia kwa ujumla.

“Kwa mafanikio tuliyopata hadi sasa, tunaendelea vizuri na Iran si tishio tena kama ilivyokuwa awali,” alisema Trump. “Hii ni uwekezaji kwa usalama wa vizazi vijavyo.”

Hata hivyo, rais huyo alisisitiza kuwa vita hivyo vitaendelea hadi malengo yote ya kijeshi yatakapofikiwa kikamilifu.

“Ndani ya wiki mbili hadi tatu zijazo, tutawapiga kwa nguvu kubwa sana,” alisema. “Tutawarudisha katika hali ya nyuma kabisa ya maendeleo.”

Trump pia alitoa onyo kali kwa Iran, akisema kuwa iwapo haitakubali makubaliano na Marekani, basi mashambulizi yatapanuliwa zaidi na kulenga miundombinu muhimu ikiwemo vituo vya kuzalisha umeme.

Katika hotuba hiyo, Trump alitetea uamuzi wa kuanzisha vita hiyo, akidai kuwa Iran imekuwa ikivuruga utulivu wa dunia kwa muda mrefu na kuendelea kuendeleza mpango wake wa silaha za nyuklia.

“Dunia nzima imekuwa ikisema Iran haipaswi kuwa na silaha za nyuklia, lakini maneno pekee hayatoshi bila hatua,” alisema.

Licha ya kauli hiyo, taarifa za kijasusi zimekuwa zikitofautiana na baadhi ya madai ya Trump, hususan kuhusu uwezo wa Iran kutengeneza makombora yanayoweza kufika Marekani.

Wakati huo huo, vita hiyo imeanza kuleta athari za kiuchumi ndani ya Marekani na duniani kote, huku bei za mafuta na gesi zikiongezeka na masoko ya hisa kushuka Trump alikiri kuwepo kwa wasiwasi miongoni mwa Wamarekani kuhusu hali hiyo, lakini akailaumu Iran kwa kusababisha hali hiyo.

Kwa upande wa kijeshi Wizara ya Ulinzi ya Marekani imesema hadi sasa zaidi ya malengo 12,300 yameshambuliwa yakiwemo vituo vya makombora, maghala ya silaha na miundombinu ya kijeshi ya Iran.

10YrsJembefm  #Familiamoja #AhsantekwaTime

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii