Waandishi wa habari Philimon Mawazo na Leah Mnyambwa wamekamatwa na Jeshi la Polisi mjini Musoma mkoani Mara wakati wakiripoti taarifa za mkutano uliokuwa umeandaliwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) katika maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani, uliokuwa umepangwa kufanyika leo Jumapili, Machi 8, 2026.
Akizungumza kuhusiana na tukio hilo, Meneja wa Watangazaji wa Kituo cha Jembe FM Mwanza, Albert G. Sengo, amesema amesikitishwa na kukamatwa kwa wanahabari hao wakati wakitekeleza majukumu yao ya kihabari.
G. Sengo amesema waandishi hao walikuwa wakifanya kazi yao halali ya kuhabarisha umma, kama ambavyo askari polisi walivyokuwa wakitekeleza majukumu yao ya kiusalama, hivyo hakutarajia kuona wanahabari wakikamatwa.
Amesema wanahabari wana mchango mkubwa katika kuelimisha na kuifahamisha jamii kuhusu matukio yanayoendelea, na hivyo ameliomba Jeshi la Polisi kuwaachia mara moja bila masharti.
“Ombi letu la msingi ni Jeshi la Polisi kuwaachia mara moja bila masharti, kwa sababu waandishi wa habari walikuwa kazini na kazi yao inatambulika kisheria,” amesema G. Sengo.
Ameongeza kuwa kuwakamata waandishi wa habari wakati wanatekeleza majukumu yao ni kitendo kisichowatendea haki.
Taarifa zinaeleza kuwa wanahabari hao walikamatwa nje ya viwanja vya Kanisa Katoliki Parokia ya Mwembeni, Musoma Mjini, ambako mkutano huo wa CHADEMA ulidaiwa kupangwa kufanyika kabla ya kusitishwa.
Wakati huo huo, juhudi za kumpata Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Pius Lutumo, ili kutoa ufafanuzi juu ya tukio hilo bado zinaendelea.