Ndege ya kijeshi iliyokuwa na watu 121, wengi wao wanajeshi, ilianguka muda mfupi baada ya kupaa jana Jumatatu huko Puerto Leguizamo, Colombia, na kuua watu wasiopungua 33.
Naibu wa meya wa mji huo Carlos Claros amesema karibu watu 81 walijeruhiwa katika mkasa huo. Mji wa Puerto Leguizamo uko Putumayo, jimbo la Amazon linalopakana na Equador na Peru. Waziri wa Ulinzi Pedro Sánchez alisema kwenye mtandao wa X kwamba ndege iliyoanguka Jumatatu ilikuwa ikiwasafirisha wanajeshi hadi mji mwingine huko Putumayo.
Sánchez alisema kuwa hadi sasa hakuna dalili zozote zinazoonyesha kwamba ndege hiyo ilishambuliwa na makundi ya waasi yanayoendesha harakati zao karibu na Puerto Leguizamo nchini Colombia. Jeshi la anga lilisema katika taarifa kwamba kiasi ya watu 77 waliokolewa kutoka eneo la ajali wakiwa na majeraha.
Msemaji kutoka Wizara ya Ulinzi alisema kwamba maafisa bado wanachunguza idadi ya mwisho ya vifo. Vyombo vya habari vilisambaza video za wanajeshi wakiondolewa haraka kutoka eneo hilo kwa pikipiki zilizoendeshwa na wakazi wa eneo hilo, huku kundi lingine la wakaazi likijaribu kuzima moto ambao ndege hiyo ilisababisha katika uwanja uliozungukwa na majani mengi.
10YrsJembefm #Familiamoja #AhsantekwaTime