Fahamu historia ya Mti wa Araucaria ssp Uliopandwa na Nyerere mwaka 1989

Mti wa Araucaria spp ni miongoni mwa miti ya jamii ya misonobari (conifers), inayojulikana kwa umbo lake la kuvutia lenye matawi yanayopangwa kwa mpangilio wa duara kuanzia chini hadi juu.

Miti hii hukua kwa urefu mkubwa na hudumu kwa muda mrefu, jambo linaloifanya kuwa bora kwa mapambo na kumbukumbu ingawa asili yake inatokana na maeneo ya kusini mwa dunia, hasa nchi kama Australia, New Caledonia na Amerika ya Kusini .

Nchini Tanzania, miti ya Araucaria hupandwa zaidi katika maeneo yenye hali ya hewa ya baridi kiasi na mvua za kutosha ambapo mikoa inayojulikana zaidi kwa uwepo wake ni:
Iringa hasa maeneo ya nyanda za juu kama Mafinga ,Njombe,Kilimanjaro , (hasa maeneo ya milimani) pamoja na Arusha .

Katika jamii nyingi miti ya Araucaria hutumika kwa kupendezesha mazingira, kutoa kivuli, pia kama alama ya kumbukumbu katika matukio maalum.

Aidha miti hii hupendelewa sana na taasisi, shule, makanisa na hata familia, hasa wakati wa sherehe kama Krismasi kutokana na muonekano wake unaofanana na mti wa Krismasi.

Mti wa Araucaria spp ni miongoni mwa mti uliyopata bahati ya kupandwa na Baba wa Taifa  ka Tanzania Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere mnamo tarehe 04 Agosti nwaka 1989 katika eneo ka Shamba la miti la Sao Hill lililopo Mafinga Mkoani Iringa linalomilikiwa na wakala wa Uhifadhi Mistu TFS.

  Ingawa tukio hilo ni sehemu ya historia muhimu ya juhudi za Tanzania katika kulinda mazingira na kuhimiza utamaduni wa upandaji miti linaweza kuonekana dogo kwa nje lakini  lina uzito mkubwa katika kueleza falsafa ya uongozi wa Nyerere iliyojikita katika uwajibikaji kwa vizazi vya sasa na vijavyo.

Katika kipindi cha uongozi wake na hata baada ya kustaafu urais mwaka 1985, Nyerere aliendelea kuwa mstari wa mbele kuhamasisha uhifadhi wa mazingira.

Aliamini kuwa rasilimali za asili kama misitu ni urithi wa taifa, hivyo zinapaswa kulindwa kwa manufaa ya baadaye.

Kupitia kauli mbiu mbalimbali na vitendo binafsi, aliwahimiza wananchi kupanda miti na kuitunza, jambo lililosaidia kuanzisha utamaduni wa kitaifa wa upandaji miti.

Kupandwa kwa mti huo wa Araucaria mwaka 1989 kulikuwa sehemu ya mwendelezo wa kampeni za kitaifa za upandaji miti zilizokuwa zikifanyika kuanzia miaka ya 1970.

Miti ya aina hii huchaguliwa mara nyingi kwa sababu ya uimara wake, ukuaji wa muda mrefu na thamani yake ya mapambo, hivyo hutumika kama alama ya kudumu ya kumbukumbu. Katika muktadha huo, mti huo uliwakilisha si tu tendo la kupanda mti, bali pia ujumbe wa kudumu kuhusu umuhimu wa kuhifadhi mazingira.

Aidha, miti ya kumbukumbu kama hii hupandwa ili kuadhimisha matukio muhimu au uwepo wa viongozi mashuhuri katika maeneo fulani kama shule, taasisi au maeneo ya umma.

Hivyo, mti wa Araucaria uliopandwa na Nyerere unapaswa kutazamwa kama “kumbukumbu hai” inayobeba historia, maadili na mafunzo kwa vizazi vijavyo kuhusu wajibu wa kulinda mazingira.

Kwa ujumla, tukio la kupandwa kwa mti huo linaakisi dhamira ya dhati ya Nyerere katika kujenga taifa linalojali mazingira. Ni mfano halisi wa uongozi unaoonyesha vitendo, na hadi leo mti huo unabaki kuwa ishara ya urithi wake katika uhifadhi wa mazingira nchini Tanzania.

Na: Gloria Kiwia 

10YrsJembefm  #Familiamoja #AhsantekwaTime

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii