Baa Marekani zaondoa pombe kali ya Russia

Baa nchini Marekani zimeondoa pombe kali aina ya vodka kutoka Russia na sasa zimebuni kinywaji kipya chotara (cocktail) kilichopewa jina la “Kyiv Mule”.

Wanywaji wa baa za michezo za Bethesda, Maryland wanaweza kupata kinywaji cha cocktail chenye mchanganyiko wa vodka, tangawizi na limao, lakini kwa jina jingine; Kyiv Mule kuenzi jiji hilo la Ukraine iliyovamiwa na majeshi ya Russia.

Ronnie Heckman, mwenye umri wa miaka 31 anayemiliki mgahawa nje ya Washington DC, alisema ameamua kuacha kununua vodka ya Russia kuonyesha mshikamano na Ukraine iliyovamiwa na Russia na kuibua mgogoro uliotikisa dunia.

“Tunatumaini kwamba watu wengine… wataungana nasi kuendelea kuelimisha kile kinachoendelea kwa sasa,” alisema Heckman, ambaye familia yake ina vinasaba vya nchi zote za Ukraine na Russia kutoka vizazi vilivyopita.

Nyuma ya baaHeckman amening’iniza Kyiv Mule pamoja na kinywaji cha Ukraine cha White or Black badala ya vinywaji vya Russia, huku sehemu ya mapato ya mauzo ya vinywaji hivyo ikienda kwenye Mfuko wa Dharura wa Kusaidia Watoto wa Ukraine.

Vodka ya Russia haijatawala soko la vinywaji vikali Amerika ya Kaskazini, lakini kwa mamlaka za Marekani na Canada kuondoa bidhaa za Russia kutoka makatini ni ishara kubwa ya kuiunga mkono Ukraine na kuungana na jumuiya ya kimataifa kupinga uvamizi wa Russia.

Heckman si mtu pekee aliyechukua msimamo huo, huku, hoteli, migahawa na baa zikifuata mkondo wa kuondoa vodka ya Russia kuanzia mji wa Kansas hadi Vermont.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii