Mwanafunzi wa Udaktari Ajipandikiza Kifaa cha Bluetooth Sikioni Kuiba Mtihani.

Mwanafunzi wa mwaka wa mwisho wa udaktari anachunguzwa baada ya kudaiwa kufanya udanganyifu katika mtihani kwa kuweka kifaa cha Bluetooth kwenye sikio lake, kulingana na afisa wa chuo kikuu.
Ripoti zilidai kwamba mtihani huo ulikuwa jaribio la mwisho kwa mwanafunzi huyo baada ya kurudia mara kadhaa tangu ajiunge na chuo hicho miaka 11 iliyopita.
Mwanafunzi huyo anayesomea udaktari katika chuo kikuu cha kibinafsi, alikuwa akifanya mtihani huo katika Chuo cha Mahatma Gandhi Memorial wakati alipatikana na simu ya mkononi kwenye mfuko wa ndani wa suruali yake iliyounganishwa na kifaa cha Bluetooth, kulingana na Mkuu katika Chuo cha Matibabu, Sanjay Dixit.
Gazeti la The Independent liliripoti kuwa wakuu wa chuo hicho walishindwa kupata kifaa cha Bluetooth walipokuwa wakimkagua mwanafunzi huyo ambaye jina lake lilibanwa.
Dixit alisema mwanafunzi huyo alikuwa akifanya mtihani wa General Medicine siku ya Jumatatu, Februari 21, 2022, wakati msimamizi wa nje wa mtihani huo na kikosi chake walipofika katika shule hiyo bila kutarajiwa na kumpata mwanaafuni mmoja na simu na mwingine akiwa na kifaa cha Bluetooth.
Dixit alisema kuwa wanafunzi hao walificha vifaa hivyo makusudi kwa sababu walitakiwa kuwasilisha vifaa vyote vya kielektroniki walivyo navyo kwa wasimamizi.
Naibu msajili, Rachna Thakur ambaye alikuwa pamoja na wakaguzi wa nje alisema kuwa baada ya uchunguzi kukamilika, itaamuliwa iwapo kesi hiyo itawasilishwa kwa polisi.
Mkuu wa kikosi cha wasimamizi, Renu Jain alisema vipaza sauti vilipandikizwa kwenye masikio ya wanafunzi wote wawili kupitia upasuaji.
Alisema kesi inaendelea dhidi ya wanafunzi wote wawili, akisema kwamba Kamati ya DAVV itatoa uamuzi katika kesi hii.
Visa vya wanafunzi kunaswa wakifanya udanganyifu katikaa mitihani kupitia njia za ujanja si jambo la geni nchini India ambako kuna ushindani mkubwa kwani watahiniwa huzidi idadi ya nafasi za kazi na viti katika vyuo vya masomo.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii