Wakenya mtandaoni wamewasifu marubani wawili wanaofanya kazi katika shirika la ndege la Kenya Airways, ambao walitua ndege huku kukiwa na dhoruba ya Eunice barani Ulaya.
Mmoja wa marubani, Ruth Karauri, alitua kwenye uwanja wa ndege wa Heathrow London huku Clive Nyachieo akitua katika uwanja wa ndege wa Amsterdam wa Schiphol.
Kutua kwa Bi Karauri kulirekodiwa na huduma ya ya upeperushaji wa moja kwa moja wakati ndege zikitua katikati ya dhoruba hiyo - ambayo ilitazamwa na mamilioni ya watu.
Rubani wa Kenya baadaye alirekodi video kwenye chumba cha marubani na afisa wake wa kwanza Ayoob Harunany, akielezea jinsi walivyotua.
Kutua kwa Bw Nyachieo kulitokea muda mfupi baada ya ndege ya mizigo kuacha kutua katika uwanja wa ndege wa Schiphol kwa sababu ya hali mbaya ya hewa.
Wakenya mtandaoni wikendi nzima wamewasifu marubani wote wawili.
"#StormEunice pia iliathiri sehemu kubwa ya Uropa na Kapteni Clive Nyachieo alifanya kazi nzuri kutua 787 huko Amsterdam. Hongera!," Gavana wa Benki Kuu ya Kenya Patrick Njoroge alisema."Salamu kwa Kapteni Ruth Karauri. Anawapa motisha wasafiri wa ndege huko nje kwamba inawezekana bila kujali jinsia. Salamu kwa Kenya Airways kwa kuwatoa watu stadi na wenye ujuzi," Manuel.