Familia za waathiriwa wa maandamano kuandamana hadi ikulu ya rais kudai haki

Familia za waathiriwa wa maandamano ya kupinga serikali zimetangaza nia yao ya kuandamana hadi ikulu ya rais leo Jumatatu, Desemba 22, kuomba mkutano na Rais William Ruto ili kukemea ucheleweshaji katika mfumo wa haki na ukosefu wa uwajibikaji.

Familia hizo zimetuma taarifa rasmi kwa polisi zikiwafahamisha kuhusu maandamano yao na kubainisha njia iliyopangwa.

Kulingana na taarifa hii, familia hizo zimebainisha kwamba zitaondoka Jeevanjee Gardens saa 3:00 asubuhi, ambapo zitakusanyika kabla ya kuendelea hadi ikulu ya rais.

Familia zinamwomba rais hatimaye kusikia kilio chao.

"Tunamwomba hatimaye asikie kilio cha maumivu kutoka kwa familia zinazojiandaa kutumia Krismasi bila vicheko vya wapendwa wao," taarifa hiyo inabainisha.

Wanatumai kwamba rais ataunga mkono familia za waathiriwa wa maandamano ya kupinga serikali.

Familia hizo pia zimebainisha katika taarifa hiyo kwamba zitajadili masuala ya haki na mkuu wa nchi atakapofika katika ikulu ya rais.

Wameifahamisha polisi kwamba maandamano hayo yatakuwa ya amani na kuomba polisi iweze kusindiza familia hizo.

Katika taarifa yao kwa polisi, familia hizo zilmebainisha kuwa washiriki katika maandamano hayo wangebeba maua na bendera ya taifa pekee.

"Tafadhali kumbuka kuwa haya ni maandamano ya amani; washiriki wangebeba maua na bendera ya taifa pekee," taarifa hiyo imesema.

Mapema mwaka huu, Rais Ruto alianzisha jopo la wataalamu la watu 18 ili kuratibu fidia kwa waathiriwa wa maandamano ya kupinga serikali na vurugu za polisi kuanzia mwaka 2017.

Hata hivyo, mnamo Desemba 4, Mahakama Kuu ilitangaza jopo hilo kuwa kinyume cha katiba, ikitoa uamuzi kwamba mamlaka yake ilikiuka mamlaka ya kikatiba ya Tume ya Kitaifa ya Haki za Binadamu ya Kenya (KNCHR).

#10YrsJembefm  #Familiamoja #AhsantekwaTime

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii