Serikali ya Rwanda imefunga zaidi ya makanisa 10,000 ya kiinjili nchini humo baada ya kubainika kushindwa kutimiza masharti ya kisheria yaliyowekwa mwaka 2018 kwa lengo la kudhibiti na kusimamia maeneo ya ibada.
Sheria hiyo inahusisha masuala ya afya, usalama, uwazi wa kifedha pamoja na vigezo vya elimu, ambapo inamtaka kila mhubiri kuwa na mafunzo rasmi ya kitheolojia.
Aidha, makanisa yote yanatakiwa kuwasilisha mipango ya kila mwaka inayoeleza namna yanavyofuata maadili ya taifa, huku michango ya waumini ikihitajika kupitishwa kupitia akaunti zilizosajiliwa kisheria.
Aidha Paul Kagame ameendelea kuonyesha msimamo mkali dhidi ya kuenea kwa kasi kwa makanisa ya kiinjili, hasa katika nchi za ukanda wa Maziwa Makuu ya Afrika.
Akizungumza na waandishi wa habari mwezi uliopita, Kagame alieleza wasiwasi wake kuhusu mchango wa makanisa hayo katika maendeleo ya taifa.
Aliongeza kuwa baadhi ya makanisa hayachangii maendeleo ya jamii na badala yake yamekuwa yakihusishwa na vitendo vya udanganyifu na unyonyaji wa waumini.
Hatua ya kuyafunga makanisa hayo imezua mjadala mpana ndani na nje ya Rwanda kuhusu uhuru wa kuabudu dhidi ya wajibu wa kufuata sheria za nchi.
#10YrsJembefm #Familiamoja #AhsantekwaTime