Guinea Bissau" Jeshi lachukua udhibiti wa nchi, Rais ondolewa madarakani"

Nchini Guinea-Bissau jeshi limechukua udhibiti wa nchi hiyo ambayo imekuwa ikikabiliwa na mvutano wa kisiasa baada ya rais na mpinzani wake kwenye uchaguzi wa Jumapili kujitangaza washindi katika uchaguzi huo.Aidha jeshi limetangaza kufungwa kwa mipaka ya nchi hiyo.

Milio mikali ya risasi ilisikika karibu na ikulu ya rais na makao makuu ya Tume ya uchaguzi mapema Jumatano mchana, huku watu waliovalia sare za kijeshi wakilinda barabara kuu inayoelekea kwenye ikulu.

Jenerali Denis N'Canha, Mkuu wa Ofisi ya jeshi la rais, aliwaambia waandishi wa habari kwamba amri ilitolewa kwa idara ya Jeshi kuchukuwa udhibiti wa nchi kwa muda usiojulikana hadi pale agizo litakapotolewa tena.

Rais Umaro Sissoco Embalo, ambaye aliwania urais katika uchaguzi wa Jumapili iliyopita, alikamatwa na kuzuiliwa pamoja na mkuu wa majeshi na waziri wa mambo ya ndani.

Aidha Kiongozi wa upinzani Domingos Simoes Pereira, ambaye alizuiwa kuwania uchaguzi wa urais na Mahakama ya Juu, pia alikamatwa.

Pereira alimuunga mkono mgombea wa upinzani Fernando Dias. Dias na Embalo walijitangaza washindi katika kinyang'anyiro cha urais, huku matokeo rasmi yakitarajiwa kutangazwa leo.

Guinea-Bissau imekumbwa na mapinduzi manne tangu uhuru, pamoja na majaribio mengi ya mapinduzi.

#10YrsJembefm  #Familiamoja #AhsantekwaTime


Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii