Mahakama ya Makadara iliyopo Nairobi nchini Kenya, imemhukumu kifungo cha miezi nane gerezani mwanamke Mary Ambeza baada ya kumkuta na hatia ya kudanganya kwamba ametekwa nyara na watu wasiojulikana.
Hakimu Hellen Onkwany amesema mahakama imejiridhisha kwamba mwanamke huyo alidanganya taarifa za kutekwa kwake baada ya kumtumia ujumbe mumewe, Dominic Otieno akijifanya kuwa ndiye mtekaji ambapo baada ya kufikishwa mahakamani, amekiri kwamba alidanganya kuhusu kutekwa kwake.
Tukio hilo la aina yake, lilitokea Februari 7, mwaka huu ambapo mwendesha mashtaka wa serikali aliieleza mahakama kuwa mwanamke huyo aliondoka nyumbani kuelekea kazini lakini hakurudi na ilipofika majira ya saa tatu usiku, alimtumia mumewe meseji kupitia namba yake ya simu iliyosomeka ‘Njoo uchukue mwili wa mkeo’.
Baada ya kupata ujumbe huo, mwanaume huyo alienda kuripoti katika Kituo cha Polisi cha Dandora, Eneo la Kamkunji jijini Nairobi ambapo polisi walianza upelelezi wao na baadaye, ndipo ilipobainika kwamba mwanamke huyo hakuwa ametekwa bali alidanganya.