Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limepokea magari manne mapya aina ya Robur Armored TLC300 ukiwa ni mgao kutoka kwa Mkuu wa Jeshi hilo nchini.
Akizungumza mara baada ya kupokea magari hayo Oktoba 23 mwaka huu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Benjamin Kuzaga amemshukuru Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP Camillus Wambura na Rais wa Tanzania Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa vitendea kazi hivyo ambavyo vitakavyotumika kuimarisha ulinzi na usalama wa raia na mali zao mkoani humo.
Kamanda Kuzaga amesisitiza kuwa magari hayo yatatumika kikamilifu katika kubaini, kuzuia na kutanzua uhalifu ndani ya Mkoa na kuahidi kuyatunza ili kutimiza malengo yaliyokusudiwa na Jeshi la Polisi na Serikali.
Itakumbukwa kuwa mkoa wa Mbeya utakuwa mkoa wa kwanza kupata mgao wa magari hayo ambayo yametolewa kwa ajili ya kuimarisha ulinzi na usalama.