Mkuu wa Wilaya ya Handeni Salum Nyamwese amesema Serikali imetenga Shilingi milioni 530 kwa ajili ya ujenzi wa wodi mpya ya wazazi katika Hospitali ya Halmashauri ya Mji Handeni hatua inayolenga kuboresha huduma za afya kwa kina mama na watoto.
Akizungumza leo wakati wa uzinduzi wa Bodi ya Afya ya Halmashauri ya Mji Handeni pamoja na Kamati za Usimamizi wa Huduma za Afya Nyamwese ameipongeza Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuboresha sekta ya afya nchini ikiwemo kusogeza huduma karibu na wananchi.
Nyamwese amesisitiza umuhimu wa uadilifu uwazi na uwajibikaji miongoni mwa wajumbe wa bodi, akiwataka kushirikiana na wataalamu wa afya bila kuingilia majukumu yao ya kitaalamu.
Aidha ameielekeza bodi mpya kushughulikia changamoto za ukosefu wa ushirikiano kati ya wataalamu wa afya na jamii, sambamba na uhaba wa watumishi katika vituo vya afya.
“Bodi hii ni macho na masikio ya sekta ya afya Handeni, Tushirikiane kuhakikisha huduma bora zinapatikana, na Serikali imetenga Shilingi milioni 530 kwa ajili ya ujenzi wa wodi mpya ya wazazi ili kuimarisha huduma za afya ya mama na mtoto,” amesema Nyamwese.
Pamoja na hayo, amewahimiza wajumbe wa bodi na wananchi kwa ujumla kujitokeza kwa wingi kupiga kura katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 29 mwaka huu huku akisisitiza kudumisha amani na usalama katika kipindi chote cha uchaguzi.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Handeni Maryam Ukwaju ameishukuru Serikali kwa kuendelea kutenga fedha za kuboresha huduma za afya, akibainisha kuwa Handeni ni miongoni mwa halmashauri chache zilizopata fedha za ukarabati wa hospitali mara mbili mfululizo.
Aidha ameeleza kuwa Halmashauri ina vituo 18 vya kutolea huduma za afya na inahudumiwa na watumishi 216, sawa na asilimia 44 ya mahitaji yote.
Awali Mganga Mkuu wa Hospitali hiyo Dk. Hudi Muradi amesema bodi hiyo imeundwa kwa lengo la kuimarisha usimamizi na utoaji wa huduma bora kwa wananchi ikiwa ni chombo muhimu katika kufanya maamuzi ya kimkakati katika sekta ya afya ya Halmashauri.
Kadhalika amesema tangu mwaka 2021 Halmashauri imepokea zaidi ya wahudumu wa afya 120 wa ngazi ya Kata ili kuimarisha utoaji wa huduma huku Bohari ya Dawa (MSD) ikisambaza dawa na vifaa tiba vyenye thamani ya zaidi ya Shilingi milioni 389 mwaka uliopita wa fedha. Kwa mwaka wa fedha 2025/26 Halmashauri imepanga kutumia Shilingi milioni 300 kutoka Serikali Kuu kununua vifaa tiba vya kisasa.