Mkurugenzi wa Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi (PPPC) David Kafulila amesema kuwa katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan sekta ya kilimo imepata maendeleo makubwa ambapo eneo la umwagiliaji limeongezeka kutoka hekta 540,000 hadi kufikia hekta milioni moja.
Kafulila alitoa kauli hiyo wakati wa Kongamano la Kitaaluma la Kujadili Utekelezaji wa Uchumi Jumuhishi kuelekea Dira ya Maendeleo 2050 lililoandaliwa na Chuo Kikuu cha Mzumbe (MUM) kwa kushirikiana na PPPC mjini Morogoro.
Akizungumzia sekta ya madini Kafulila alisema hapo awali sekta hiyo ilionekana kunufaisha zaidi wachimbaji wakubwa na wawekezaji wa kigeni, lakini hatua ya Rais Samia kubadilisha hati kubwa za umiliki wa migodi na kuwapa wachimbaji wadogo takribani 2,600 imeongeza mchango wao katika pato la sekta ya madini kutoka asilimia 20 mwaka 2021 hadi kufikia asilimia 40 mwaka 2024.
“Hii imeongeza ushiriki wa wananchi wa kawaida katika sekta ya madini na kuondoa malalamiko kwamba ni sekta ya wageni na watu wenye mitaji mikubwa,” alisema Kafulila.
Kuhusu sekta ya umeme, Kafulila alisema wakati Rais Samia anaingia madarakani, miundombinu ya usafirishaji umeme ilikuwa na urefu wa kilomita 6,000 pekee iliyojengwa kwa zaidi ya miaka 60 lakini katika kipindi cha miaka minne pekee imeongezeka kwa kilomita 2,000 sawa na asilimia 30 ya yote iliyojengwa tangu uhuru.
Kwa upande wake Mchumi na Mwanazuoni Dk. Bravious Kahyoza, alisema tangu mwaka 2021 uwiano wa biashara na pato ghafi la taifa ulikuwa asilimia 27 lakini hadi sasa umefikia asilimia 43 ishara kuwa shughuli za kiuchumi na biashara zimeongezeka.
Ameongeza kuwa katika kipindi hicho sekta ya umma imeboreshwa kwa kuajiri zaidi ya watumishi 400,000 jambo linaloifanya Tanzania kuongoza ukanda wa Afrika Mashariki katika ongezeko la ajira.
“Kwa mfano, katika kipindi hicho hicho, Kenya imeajiri watu 311,000, Uganda 196,000 na Rwanda watu 20,000 pekee,” alisema Dk. Kahyoza.
Naye Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mzumbe na Mtaalam wa Ubia wa Sekta ya Umma na Binafsi (PPP) Moshi Derefa alisema duniani kote miradi mingi ya maendeleo sasa inatekelezwa kwa kutumia mfumo wa ubia, unaoshirikisha sekta binafsi kuchangia kwa kutumia rasilimali fedha, teknolojia na uzoefu walionao.
“Tuna imani kubwa na sekta binafsi kwa kuwa wanakuwa mbele kiteknolojia na kiujuzi Ubia huu unafungua milango kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kushiriki katika utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo,” alisema Moshi.