Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati Dkt. James Mataragio ameliagiza Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Kampuni yake Tanzu ya Uendelezaji Jotoardhi (TGDC) kuhakikisha kuwa vifaa vyote vya uhakiki wa rasilimali Jotoardhi katika mradi wa Ziwa Ngozi vinafika kwa wakati ili kazi za uhakiki ziweze kumalizika kulingana na muda uliopangwa.
Dkt. Mataragio ametoa maagizo hayo Oktoba 22 mwaka huu wakati wa ziara yake ya kukagua kazi zinazoendelea kutekelezwa katika mradi huo wilayani Rungwe mkoani Mbeya.
“Huu mradi mnapaswa kuukamilisha kwa wakati kutokana na umuhimu wake nchini, tunapotekeleza miradi hii ya Jotoardhi tukumbuke kuwa tunatekeleza pia Sera ya Taifa ya Nishati ya Mwaka 2015 ambayo inasema Tanzania inapaswa izalishe umeme kwa kutumia vyanzo mchanganyiko (generation mix) ambapo jotoardhi ni mojawapo." Amesema Dkt. Mataragio
Kuhusu suala la vifaa vya uhakiki kuchelewa kufika katika eneo la mradi la Ziwa Ngozi ambalo litazalisha umeme wa megawati 70, Dkt. Mataragio ameagiza kuwa vifaa vyote vya mradi vinunuliwe na kufika eneo la mradi kwa mara moja.
Dkt. Mataragio ameeleza kuwa utekelezaji wa miradi ya Jotoardhi imeainishwa pia katika Mpango wa Taifa wa Nishati (National Energy Compact) ambao unaishia 2030 ambapo Tanzania inatakiwa kuwa na megawati 130 zinazotokana na rasilimali ya jotoardhi, pia Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050 inaelekeza nchi kuwa na vyanzo mchanganyiko vya kuzalisha umeme.
Aidha Kwa upande wake Meneja Mkuu wa TGDC Mha. Mathew Mwangomba ameeleza kuwa maagizo yaliyotolewa na Serikali yatatekelezwa kwa ufanisi ili kukamilisha mradi kwa wakati.
Hata hivyo akielezea maendeleo ya uhakiki wa rasilimali jotoardhi katika mradi huo, Mha. Mwangomba amesema umefikia asilimia 60 ili kuweza kufikia hifadhi ya jotoardhi.