Serikali kutumia mitambo ya TEMDO kuongeza thamani mazao

Serikali ipo katika hatua za mwisho za kukamilisha mitambo ya kuchakata na kuongeza thamani mazao ya kilimo ikiwemo Mtambo mdogo wa kuzalisha sukari ulipo Wilaya ya Busega Mkoani Simiyu unaotarajiwa kuanza kufanya kazi Machi 2026 kwa lengo la kuchochea uzalishaji na kuongeza kipato kwa wakulima wadogo.

‎Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Bw. Gerald Mweli Oktoba 20 mwaka huu baada ya kutembelea karakana ya uzalishaji mitambo katika Taasisi ya Uhandisi na Usanifu Mitambo Tanzania (TEMDO) iliyotengeneza Mtambo huo kwa lengo la kuona ni jinsi gani Wizara yake inaweza kushirikiana na Shirika hilo katika kuwawezesha Wanawake na Vijana walio chini ya Programu ya Kujenga Kesho iliyo bora.

Aidha Bw. Mweli amesema Wizara yake pamoja na taasisi zilizochini yake zitaendelea kushirikiana na TEMDO kwa kutumia mitambo mbalimbali ya kuongeza thamani mazao ikiwemo Mtambo mdogo wa kuzalisha sukari wenye uwezo wa kuzalisha Tani 20 kwa siku ili kutimiza Malengo ya Serikali ya Awamu ya Sita katika kuongeza ajira na kipato kupitia Kilimo. 

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TEMDO Profesa Frederick Kahimba na Mkurugenzi Mkuu wa Kituo cha Zana za Kilimo na Teknolojia Vijijini (CAMARTEC) wamesema Taasisi zao ziko tayari kushirikiana na Wizara ya Kilimo na Taasisi zake kwa kutengeneza mitambo yoyote itakayohitajika pamoja na kutoa ushauri wakitaalamu na matengenezo ya mitambo pale yanapohitajika 

‎Naye Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Nafaka na Mazao Mchanganyiko Bi Irene Mlola, Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko (CPB), Bw. Patrick M. Mongella pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Kahawa Tanzania Bw. Primus Kimaryo, wameahidi kuendelea kushirikiana na TEMDO katika kuendeleza teknolojia za viwanda vinavyolenga kuwasaidia wakulima kuongeza tija.

Vilevile Mkurugenzi wa usanifu na utafiti wa TEMDO Mhandisi Nicas Bernard amesema kuwa anaona Faraja Taasisi yake ikifanikiwa kutatua changamoto mbalimbali kwa kutumia ubunifu na teknolojia kwa kutengeneza mitambo kulingana na mahitaji ya Wateja.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii