Waziri Kombo akutana na mabalozi wa Nordic kujadili namna ya uwekezaji

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo amekutana na Mabalozi wa nchi za Nordic walioko nchini Tanzania kwa lengo la kuimarisha ushirikiano wa maendeleo, uwekezaji na biashara endelevu.

Kikao hicho kimefanyika jijini Dar es Salaam kufuatia Mkutano wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Afrika na Nordic uliofanyika Victoria Falls, Zimbabwe tarehe 2 na 3 Oktoba  mwaka huu.

Akizungumza katika kikao hicho Waziri Kombo aliishukuru Nordic kwa uhusiano wa muda mrefu ulioanza tangu Tanzania ilipopata uhuru akibainisha kuwa Tanzania imeendelea kunufaika na misaada na miradi ya sekta za elimu, nishati, afya, utawala bora na umeme vijijini.

Alisema mchango huo umejenga msingi wa uhusiano wa kuaminiana na ushirikiano wenye manufaa kwa wananchi.

Waziri Kombo alieleza kuwa Serikali imezindua Mkakati wa Ushirikiano wa Tanzania na Nordic unaolenga kuimarisha diplomasia ya uchumi na kuhamasisha uwekezaji badala ya utegemezi wa misaada.

Awali aliainisha kuwa mkakati huo unalenga sekta tisa za kipaumbele, ikiwemo nishati jadidifu, miundombinu, elimu ya ufundi, uchumi wa buluu, viwanda, misitu na biashara kupitia mpango wa Aid for Trade.

Hivyo  alisema kuwa Tanzania inapanga kuvutia uwekezaji wa kati ya dola za Kimarekani bilioni 1 hadi 1.5 kutoka Nordic, pamoja na kuwasilisha miradi 17 ya kipaumbele inayotekelezwa kwa ushirikiano na TISEZA kwa ajili ya kuendeleza teknolojia, ubunifu na ajira jumuishi.

Aidha pia alitoa wito kwa taasisi za kifedha za Nordic kama Norfund, Finnfund na Swedfund kushirikiana na Serikali kuanzisha Mfuko wa Pamoja wa Ufadhili wa Uwekezaji.

Kwa upande wao mabalozi wa nchi za Nordic wameeleza dhamira ya kuendeleza uhusiano na Tanzania kwa kuhamisha mkakati kutoka mfumo wa misaada kwenda katika ushirikiano wa usawa unaolenga diplomasia ya kiuchumi.

Hata hivyo Wamesema  kuwa historia ndefu ya urafiki kati ya pande hizo mbili imeweka msingi imara wa kukuza fursa mpya za biashara uwekezaji na maendeleo ya pamoja.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii