Dodoma huduma sasa kidijitali

Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais – TAMISEMI anayeshughulikia Afya Prof. Tumaini Nagu ameipongeza Serikali ya Korea Kusini kupitia Shirika la Maendeleo la KOICA kwa mchango mkubwa katika kuboresha huduma za afya mkoani Dodoma kupitia upanuzi wa Mfumo wa GoTHOMIS.

Akifungua kikao kazi cha tathmini ya mafanikio ya utekelezaji wa mfumo huo Prof. Nagu alisema kuwa sekta ya afya mkoa wa Dodoma imeingia katika hatua mpya ya mageuzi ya kidijitali kuanzia mwaka 2022 hadi  mwaka huu hali iliyowezesha utoaji wa huduma kwa ufanisi na uwazi zaidi.

Amesema mfumo wa GoTHOMIS (Government of Tanzania Hospital Management Information System) umefanikiwa kufikia vituo 235 vya kutolea huduma za afya katika halmashauri 8 za mkoa huo na umeleta maboresho katika usimamizi wa taarifa za wagonjwa ukusanyaji wa mapato ufuatiliaji wa dawa na utoaji wa takwimu sahihi kwa maamuzi ya kitaalamu.

Prof. Nagu ameeleza kuwa kupitia mfumo huo vituo vya afya vimepunguza muda wa kuhudumia wagonjwa vimeimarisha uhifadhi wa taarifa na kuongeza uwajibikaji katika matumizi ya rasilimali hatua inayodhihirisha dhamira ya Serikali katika kujenga sekta ya afya ya kisasa inayotumia TEHAMA.

Aidha Prof. Nagu ameishukuru KOICA na wadau wengine wa maendeleo kwa kuendeleza ushirikiano na Serikali ya Tanzania, akisisitiza kuwa mafanikio yaliyofikiwa ni msingi thabiti wa uendelevu wa mfumo huo katika siku zijazo.

Mradi wa GoTHOMIS unaendelea kutajwa kama mfano bora wa mageuzi ya TEHAMA katika afya, na Dodoma sasa inaonekana kuwa kinara katika utekelezaji wa mifumo ya afya kidijitali

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii